Vieira aanza kazi kambini mwa Palace kwa ushindi dhidi ya Walsall kirafiki

Vieira aanza kazi kambini mwa Palace kwa ushindi dhidi ya Walsall kirafiki

Na MASHIRIKA

KOCHA Patrick Vieira alianza vyema majukumu yake kambini mwa Crystal Palace kwa kuongoza waajiri wake kupepeta Walsall 1-0 katika mechi ya kirafiki mnamo Jumamosi ugani Banks.

Bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo wa kujiandaa kwa msimu mpya wa 2021-22 lilifumwa wavuni na fowadi Wilfried Zaha.

Vieira ambaye ni kiungo wa zamani wa Arsenal, aliwahi kuwa kocha wa Nice katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kabla ya kuaminiwa kuwa kizibo cha mkufunzi Roy Hodgson aliyeondoka ugani Selhurst Park mwishoni mwa msimu wa 2020-21. Vieira aliajiriwa na Palace kwa mkataba wa miaka mitatu.

Hakuna mwanasoka yeyote kati ya Michael Olise na Remi Matthews ambao ni sajili wapya wa Palace waliwajibishwa na Vieira dhidi ya Walsall. Hata hivyo, beki Nathaniel Clyne alichezeshwa kwa dakika 45 za kwanza licha ya kwamba bado hajapokezwa mkataba mpya baada ya kandarasi yake ya awali kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Zaha ndiye alitamba zaidi kambini mwa Palace kwa kuwaweka waajiri wake kifua mbele katika dakika ya nne ya mchezo baada ya kushirikiana na fowadi Rob Street.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Akumu na klabu yake ya Kaizer Chiefs wapigwa kwenye fainali...

JAMVI: Raila kuvizia ziara za Rais Ukambani kwaibua hofu