Vifaranga wapya wa Raila

Vifaranga wapya wa Raila

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, amewanasa washirika wapya baada ya vinara wa vyama vikuu vya kisiasa kuapa kwamba, hawatamuunga mkono kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Washirika wake katika uliokuwa muungano wa NASA, Musalia Mudavadi (Amani National Congres, ANC,) Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetangula (Ford Kenya) wameshikilia kwamba hawawezi kumuunga Bw Odinga kwa mara ya tatu.

Watatu hao ambao wameungana kusuka muungano wa One Kenya Alliance (OKA) sasa wanasema wamemkaribisha Bw Odinga kujiunga nao bila masharti.

Inasemekana walikaa ngumu Rais Uhuru Kenyatta alipowataka wamuunge mkono waziri mkuu huyo wa zamani alipowakutanisha katika ikulu ya Mombasa Jumanne wiki hii.

Hata hivyo, Bw Odinga anaonekana kujiandaa kugombea urais bila kutegemea vigogo hao wa kisiasa na amewanasa wanasiasa chipukizi wanaotoka ngome za watatu hao.

Katika eneo la Ukambani ambalo ni ngome ya Bw Musyoka, Bw Odinga amemnasa Gavana wa Machakos Alfred Mutua kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap ambaye amekuwa akimpiga vita Bw Musyoka.

Mnamo Ijumaa, Bw Odinga aliandamana na Gavana Mutua hadi katika Kaunti ya Kiambu, wiki mbili baada ya kuandamana katika hafla nyingine Kaunti ya Murang’a.

Gavana Mutua amekuwa akishirikiana na Gavana Charity Ngilu wa Kitui na Kivutha Kibwana wa Makueni kumpiga vita Bw Musyoka.

Bi Ngilu aliyewahi kushirikiana na Bw Odinga amekuwa akiwataka viongozi wa upinzani kuungana kabla ya uchaguzi mkuu ujao ili kumshinda Naibu Rais William Ruto.

Kwenye hafla hiyo, Dkt Mutua alimwambia Bw Odinga asitishwe na kutengwa na vinara wa OKA.

“Waache wanaotaka kuenda waende. Sisi tuko tayari kuungana na viongozi wanaotaka kuchapa kazi wasio na doa,” Dkt Mutua alisema.

Katika eneo la Magharibi mwa nchi wanakotoka Bw Mudavadi na Bw Wetangula, Bw Odinga amemkumbatia kwa karibu Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa katika juhudi za kudumisha umaarufu wake eneo hilo.

Katika eneo hilo pia anamtegemea Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna na mbunge maalumu, Godfrey Otsosi ambaye amekuwa akimpigia debe.

Amewakumbatia pia magavana Wilbur Otichillo (Vihiga) na Wycliffe Wangamati (Bungoma).

Bw Sifuna anasisitiza kuwa, ODM haitishwi na misimamo migumu ya vinara wa OKA akisema, chama hicho kiko mbioni kusaka marafiki wapya.

“Hatuwezi kufungwa na marafiki wachache wanaotupatia masharti. Kama chama, tumeamua kusaka marafiki wapya kuelekea 2022,” Bw Sifuna alisema alipotangaza hatua ya ODM kujiondoa NASA.

Bw Odinga amekuwa akimchangamkia mwenyekiti wa chama cha Kanu Gideon Moi ambaye japo ni mmoja wa vinara wa OKA, anasemekana kutokuwa na msimamo mkali kama waliokuwa washirika wa waziri mkuu huyo wa zamani katika NASA.

“Ukitaja Bw Moi, huwezi kumuacha katibu mkuu wa chama hicho Nick Salat ambaye ndiye msemaji wa Kanu. Hao wawili ni tegemeo la Bw Odinga katika eneo la Rift Valley,” asema mchanganuzi wa siasa Oscar Rono.

Katika eneo la Mlima Kenya, Bw Odinga amemweka kwenye mbawa zake aliyekuwa mgombea urais Peter Kenneth ambaye wamekuwa wakiandamana kwenye hafla mbali mbali.

Duru zinasema anaendelea kuwinda wanasiasa zaidi katika eneo hilo.

Ingawa amekuwa akifurahia umaarufu mkubwa eneo la Pwani, Bw Odinga ametandaza mbawa zake na kumvua mfanyabiashara Suleiman Shahbal.

Mfanyabiashara Suleiman Shahbal. Picha/ Maktaba

Shahbal, alijiunga na ODM wiki mbili zilizopita na ananuia kutumia umaarufu wa chama hicho kugombea ugavana Kaunti ya Mombasa.

You can share this post!

Juhudi za Naibu Rais kupenya Ukambani zapata pigo kubwa

Kamishna wa Kaunti ya Nakuru aagizwa kufika Kortini