Kimataifa

Vifo kutokana na corona Italia sasa vingi kuliko China

March 20th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ROME, ITALIA

VIFO vya watu 427 kwa siku moja pekee nchini Italia saa vimelifanya taifa hilo kuipiku China kwa idadi ya waliouawa na virusi vya corona.

Kufikia sasa, Italia ina jumla ya watu 3,405 waliouawa na ugonjwa huo, ikilinganishwa na 3,245 walioaga dunia China.

Italia ilifunga miji yote na ikawaamuru raia wake wajitenge manyumbani hadi Machi 12. Sasa agizo hilo limezidishwa hadi Machi 25.

Akiongea na wanahabari wa gazeti la Corriere Della, Waziri Mkuu Giuseppe Conte alisema muda huo wa watu kukaa nyumbani ulirefushwa ili serikali iendelee kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Hata hivyo, alisema kuwa baada ya serikali kukabiliana na ugonjwa huo, raia hawataweza kurudi kikamilifu kwa mtindo wa maisha kama walivyozoea.

“Hata baada ya kukabiliana na ugonjwa huu kama taifa, hatutaweza kurudi mara moja na kuendelea na mtindo wa maisha tuliozoea awali,” alisema.

Licha ya hatua hizi, Italia bado imeendelea kushuhudia visa vipya vya maambukizi na vifo kuongezeka.

Ripoti kutoka kwa Idara ya utafiti ya Istituto Superiore di Sanita kuhusu vifo nchini, ilionyesha kuwa, watu 2,003 walithibitishwa kuugua ugonjwa huo, hasa katika eneo la Kaskazini.

Utafiti ulionyesha walioathirika zaidi ni wazee wanaoishi na jamaa zao wenye umri kati ya miaka 18 na 34.

Utafiti huo ulionyesha pia kuwa kulikuwa na uwezekano kuwa demografia tofauti katika nchi zingine zilichangia katika kupunguza kwa idadi za vifo.

Kwa jumla, kumethibitishwa visa 220,000 ulimwenguni na vifo zaidi ya 9,000.

Jumatano, serikali ya China ilitangaza kwa mara ya kwanza kuwa haikusajili visa vyovyote vipya vilivyoanzia nchini tangu kuwe na mrupuko huo.

Ingawa iliripoti visa vipya 34 vya wasafiri ambao walikuwa wamefika nchini majuzi.

China bado inaoongoza na idadi kubwa ya wagonjwa kutokana na virusi hivyo ikisajili zaidi ya visa 81,000 ilihali Italia imeripoti jumla ya wagonjwa 41,035.

Taifa la Ufaransa pia lilifunga miji yake Jumanne asubuhi na kuwaagiza raia wakae nyumbani.

Raia watakaopatikana katika maeneo ya umma watahitajika kubeba hati rasmi zikieleza kwa nini hawajitenga nyumbani la sivyo watatozwa faini.

Waziri ya Masuala ya Mambo ya Ndani Bw Christophe Castaner aliiambia redio ya Europe 1 Alhamisi kuwa, kulikuwa na uwezekano wa hatua hiyo kusukumwa zaidi ya siku 15 kinyume na serikali ilivyosema mwanzoni.

Alisema faini 4,095 zimekabidhiwa wakosaji na cheki 70,000 kudhibitiwa tangu Jumatano asubuhi.