Habari Mseto

Vifo kutokana na Ukimwi vyapungua kwa asilimia kubwa nchini Kenya

November 28th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MAAMBUKIZI ya virusi vya Ukimwi yamepungua kwa kiwango kikubwa sawa na vifo, utafiti uliofanywa majuzi umebainisha.

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki alisema imebainika ya kwamba vifo vya watu walioambukizwa virusi vinavyosababisha Ukimwi vimepungua kwa asilimia 50.

Alisema ifikapo mwaka wa 2020 serikali inataka kuona kiwango hicho kimepungua hadi kwa asilimia ya chini kabisa.

“Serikali itaendelea kuwatambua wafanyakazi wa kujitegemea katika sekta ya afya wafikao 60,000 ambao kufanya kazi mashinani ili kujumuika pamoja na wananchi,” alisema Bi Kariuki.

Aidha, alisema watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi watapewa ushauri jinsi ya kutumia dawa za kupunguza nakali – ARVs – na kupata lishe bora.

Aliyasema hayo mnamo Jumanne katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika.

Washiriki wa mkutano wa kuangazia ripoti kuhusu Ukimwi katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Mkurugenzi wa Umoja wa kimataifa kuhusu virusi vya ukimwi (UNAIDS), Bi Winnie Byanyima, alisema katika bara la Afrika, watu wapatao 25 milioni wameambukizwa virusi vya Ukimwi.

“Kulingana na utafiti uliofanywa hivi majuzi, kiwango cha walioambukizwa VVU kimepungua kwa asilimia 50 huku 24.5 milioni wakiendelea kupata matibabu,” alifafanua Bi Byanyima.

Alisema shirika hilo la Umoja wa Mataifa linataka kuona ya kwamba ifikapo mwaka wa 2030 maradhi ya Ukimwi inaangamizwa kabisa.

Utafiti uliofanywa umebainisha kuwa wanawake na wasichana ndio idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi.

Ilidaiwa kuwa wao ndio hushughulika na kazi nyingi za nyumbani na kutekeleza majukumu mengine.

Alisema katika bara la Afrika watu kati ya umri wa miaka 16 na 24 ndio wameathirika sana kutokana na maradhi hayo, huku akiongeza ya kwamba wanawake wapatao 6,000 huambukizwa maradhi hayo kila wiki.

Naibu gavana wa Kaunti ya Kiambu, Dkt James Nyoro, alisema ufukara umeathiri eneo la Kiandutu na hivi karibuni wakazi wa kijiji hicho watapata makazi mazuri.

Alisema katika uongozi wake atafanya juhudi kuona ya kwamba hospitali za kiwango cha chini zimeboreshwa kwa kupata dawa kwa wingi.

“Nitafanya juhudi kuona ya kwamba kuna dawa za kutosha katika hospitali zote katika Kaunti ya Kiambu. Nitafanya juhudi kuona ya kwamba tunapata mabohari ya kuhifadhi dawa ili kuwe na mwongozo bora wa kusambaza dawa zenyewe,” alisema Dkt Nyoro.

Bw Stanely Njuguna ambaye ni mkazi wa Kiandutu aliiomba serikali ifanye juhudi ya kubuni kazi kwa vijana ambao wengi wao hawana ajira.

Alitaka Kaunti ya Kiambu kuinua maisha ya wakazi wa Kiandutu kwa kuwajengea vyoo na kusambaza maji safi.