Vifo vinavyotokana na kufanya kazi kwa saa nyingi vimeongezeka duniani – WHO

Vifo vinavyotokana na kufanya kazi kwa saa nyingi vimeongezeka duniani – WHO

Na MASHIRIKA

GEVENA, USWISI

MAELFU ya watu, wengi wao wakiwa wanaume, wanafariki kote duniani kila mwaka kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu kupita kiwango, utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) umebaini.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na WHO kwa ushirikiano na Shirika la Wafanyakazi Duniani (ILO) katika mataifa 154 kati ya 1970 na 2018, inasema kuwa kufanya kazi kwa muda mrefu kunasababisha maradhi ya moyo na kiharusi ambayo huua maelfu ya watu kila mwaka kote duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu milioni 450 walifanya kazi kwa zaidi ya saa 55 kwa wiki mnamo 2016 kote duniani. Kati yao, watu 745,000 walifariki kutokana na maradhi ya moyo na kiharusi.

Shirika la WHO linasema kuwa mtu anayefanya kazi kwa muda wa saa 55 na zaidi kwa wiki, yuko kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa moyo na kuugua kiharusi.

Kati ya 2000 na 2016, idadi ya vifo vilivyotokana na magonjwa ya moyo kwa sababu ya kufanya kazi kwa muda mrefu viliongezeka kwa asilimia 42, na kiharusi asilimia 19.

Asilimia 72 ya wanaokufa kwa kufanya kazi kwa muda mrefu ni wanaume.

Vifo vingi vinavyotokana na kufanya kazi kwa saa nyingi vilishuhudiwa miongoni mwa watu wa kati ya umri wa miaka 60 na 79.

Ripoti hiyo inasema vifo vya aina hiyo vimepungua kwa kiasi kikubwa katika mataifa ya Ulaya na Amerika Kaskazini kwa sababu waajiri wanazingatia saa za kazi.

Shirika la WHO linashauri kuwa mtu anastahili kufanya kazi kwa kati ya muda wa saa 35 na 40 ili kuepuka maradhi ya moyo. Muda huo ni sawa na saa nane kwa siku.

Ripoti hiyo, hata hivyo, inasema kuwa idadi ya watu wanaofanya kazi kwa muda mrefu inaongezeka kwa kasi duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, alisema kuwa janga la Covid-19 kwa kiwango kikubwa limebadili mtindo wa kufanya kazi miongoni mwa badhi ya watu.

Kufanya kazi kwa njia ya simu, Tedros alisema, kumekuwa na nafasi kubwa kwa sasa katika maeneo mengi ya viwanda.

Aliwataka waajiri na serikali kuhakikisha kuwa muda wa kazi unakuwa chini ya saa 55 ili kulinda afya ya wafanyakazi. Watu wanaofanya kazi zao za kibinafsi pia walishauriwa kuhakikisha kuwa wanapumzika.

Tafsiri: LEONARD ONYANGO

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nakumbwa na hofu kuu ya kujifungua

2022: Uhuru kujipanga upya