Bambika

Vifo vya mapema vya Maceleb Kenya vilivyoshtua

March 22nd, 2024 2 min read

NA SINDA MATIKO

IJAPO mwaka ungali mchanga, tayari vimetokea vifo kadhaa vya ghafla vya mastaa vilivyowaacha Wakenya wengi na mshangao.

Mazingira ya vifo hivyo pia yamezua gumzo sana.

Unaweza kusema vifo hivi havikutarajiwa, ila vilifanya kushtukiza tu na ndio sababu vimeweza kutrendi.

BRIAN CHIRA

(Machi 15, 2024)

Chanzo: Agongwa na lori

‘Tiktoker’ Brian Chira aliishi maisha yenye hekaheka kibao na hadi kifo kinamchukua, hekaheka zilihusika.

Chira alijipatia umaarufu kutokana na kauli zake pamoja na mienendo ya utata. Kando na kuweka wazi kwamba alikuwa ana virusi vya Ukimwi, Chira aliishi maisha ya kutojali huku akiwa mraibu wa pombe.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, kuelekea tukio la kifo chake, Chira alikuwa ametoka baa na huko alikuwa amezua zogo na kusababisha walinzi kumfurusha.

Aliabiri bodaboda kuelekea nyumbani na alipokaribia, inadaiwa alijaribu kusepa ili kukwepa kulipa nauli. Ni kwenye harakati hizo ndipo aligongwa na lori alipokuwa akijaribu kuvuka barabaraba akimkimbia mhudumu wa bodaboda. Alifariki papo hapo.

MWANAHABARI RITA TININA

(Machi 17, 2024)

Chanzo: Homa ya mapafu (Pneumonia)

Rita mwanahabari mwenye takriban miongo miwili kwenye tasnia ya uanahabari alipatikana akiwa amefariki nyumbani kwake Kileleshwa.

Kifo chake kilibainika Rita aliposhindwa kufika kazini kituo cha NTV.

Upasuaji wa mwili wake ulithibitisha kwamba alifariki usingizini baada ya kulemewa na homa ya mapafu. Kifo chake kiliiwaacha wengi hoi, na kutrendi sana kwenye mitandao ya kijamii.

KELVIN KIPTUM

(Februari 11, 2024)

Chanzo: Ajali mbaya ya barabarani

Mshikilizi wa rekodi ya dunia kwenye marathon, Kiptum alikuwa ametoka kujivinjari akirejea nyumbani alipokumbana na mauti yake.

Kiptum alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Premo abiria wengine wakiwa ni kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizamana na mwanamke kwa jina Sharon

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, gari lilikuwa kwenye kasi, Kiptum alipopoteza mwelekeo na kugonga mti. Yeye na kocha wake walifariki papo hapo Sharon akiponea.

CHARLES OUDA

(Februari 4, 2024)

Chanzo: Ajinyonga

Ni kifo kingine kilichowashtua Wakenya na kuwaacha na maswali kibao. Siku moja kabla video zilimwonyesha Charles akiwa mchangamfu sana baada ya kuhudhuria pati.

Sababu halisia za kilichopelekea kifo chake hazijawahi kuwekwa wazi ila vyanzo kadhaa vilidhibitisha kwamba alijitia kitanzi.

STARLET WAHU

(Januari 3, 2024)

Chanzo: Auawa

Modo maarufu wa Instagram alipatikana akiwa ameuawa kikatili kwenye mjengo mmoja mtaani South B.

Kamera za siri zilionyesha akiingia kwenye mjengo huo na John Matara ambaye anaaminika alikuwa ni mpenzi wake.

Ilidaiwa baada ya wawili hao kurushana roho kwa mujibu wa kondumu zilizotumika kupatikana, kulizuka zogo lililosababisha Matara kumchoma visu kadhaa na kusababisha mauti yake.

Kesi ya madai hayo ingali mahakamani.