Habari Mseto

Vifo wakati wa kujifungua vimepungua – Wizara ya Afya

October 31st, 2018 2 min read

Na ERIC MATARA

IDADI ya akina mama wajawazito wanaofariki wakijifungua nchini imeshuka, huku zaidi ya asilimia 62 ya akina mama wajawazito nchini wakipokea huduma za kiafya kutoka kwa wahudumu wenye ujuzi, rekodi za Wizara ya Afya zinaonyesha.

Hii imechangiwa na kuanzishwa kwa mipango ya Beyond Zero ulioanzishwa na Mama Taifa Margaret Kenyatta na Linda Mama iliyoanzishwa na Wizara ya Afya. Chini ya mipango hiyo, akina mama wajawazito wamekuwa wakipokea huduma maalum za afya na kwa gharama ya chini.

Kimsingi, vifo vya akina mama hao vimepungua kutoka wastani wa 488 kati ya wanawake 100,000 waliojifungua kati ya miaka ya 2008 na 2009 hadi wastani wa wanawake 362 kote nchini mwaka huu.

Kulingana na ripoti kuhusu uchunguzi wa hali ya kiafya nchini, Kenya Demographic and Health Survey, zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wajawazito nchini hupata huduma bora za kiafya.

Uimarishaji wa shughuli za utoaji chanjo, mipango ya kupambana na maradhi ya Malaria, HIV na Ukimwi, polio na maradhi mengine ambayo huwaathiri watoto, zimetajwa kama sababu zilizochangia kupungua kwa vifo hivyo.

Miaka kumi iliyopita idadi ya akina mama wajawazito waliofariki ilikuwa ya juu nchini Kenya hadi wastani wa vifo 600 kati ya wanawake 100,000 waliojifungua.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Kenya ni miongoni mwa nchini 10 ambazo zilichangia asilimia 58 ya vifo vya akina mama wajawazito duniani, kwa kuchangia asilimia mbili katika takwimu hiyo.

Kulingana na data iliyochambuliwa mnamo 2009, idadi ya juu ya vifo viliripotiwa katika uliokuwa mkoa wa Kaskazini Mashariki (2,014 kati ya wanawake 100,000 waliojifungua) ukifuatwa na Nyanza (546 kati ya wanawake 100,000 waliojifungua) huku idadi ya chini zaidi ikiandikishwa katika mkoa wa Nairobi (212 kati ya 100,000 waliojifungua).

Hata hivyo, takwimu hizo hazikuonyesha idadi ya vifo katika kila kaunti huku Waziri wa Afya Bi Cecily Kariuki akisema mengi yanapasa kufanywa kuhakikisha kuwa wanawake wote wanaojifungua wanahudumiwa na wahudumu wa afya waliohitimu.

Serikali ya Kitaifa kupitia wizara hiyo sasa inalenga kushirikiana na wafadhili ili kuzipiga jeki serikali za kaunti ili ziweze kupunguza idadi ya vifo vya akina mama wanapojifungua.

Kulingana na takwimu hizo, wizara ya afya inalenga kuimarisha huduma muhimu ya kiafya kama vile upangaji wa uzazi, huduma za kabla ya kujifungua kwa wanawake, huduma wakati wa kujifungua na huduma za baada ya kujifungua.

Kulingana na Waziri Kariuki, wizara yake inalenga kuhakikisha kuwa huduma hizo za afya zinawafikia akina mama hadi katika maeneo ya mashinani.