Vigogo Man-U, Chelsea na Liverpool mawindoni leo

Vigogo Man-U, Chelsea na Liverpool mawindoni leo

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MIAMBA wa Manchester United, Chelsea na Liverpool watalenga kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kishindo hii leo Jumamosi watakapokutana na wanyonge Leeds, Crystal Palace na Norwich mtawalia.

Red Devils wa Man-United wataalika Leeds ugani Old Trafford, Chelsea wakiwa nyumbani Stamford Bridge nao Liverpool wanafunga safari kuzuru Norwich.

Man-United hawajawahi kupoteza dhidi ya Leeds katika mechi 15 zilizopita za ligi uwanjani mwao.

Vile vile, vijana wa kocha Ole Gunnar Solskjaer hawajapoteza mara nne mfululizo katika mashindano yote.

Walikung’uta Leeds ya kocha Marcelo Bielsa 6-2 ugani Old Trafford msimu uliopita.

Red Devils watakosa huduma za wachezaji kadhaa nyota wakiwemo Marcus Rashford na Edinson Cavani, ingawa kikosi cha leo kitajumuisha mshambuliaji matata Mason Greenwood, viungo stadi Paul Pogba na Fernandes pamoja na beki Harry Maguire.

Sajili mpya Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund anaweza kuonja dakika zake za kwanza dhidi ya Leeds.

“Nimekuwa nikisubiri kwa muda mrefu uhamisho huu kufanyika, kwa hivyo nafurahi kuwa sasa niko hapa. Niko tayari kuanza msimu dhidi ya Leeds,” alisema mshambuliaji Sancho.

Leeds itakuwa bila Diego Llorente, lakini mastaa wake Raphinha, Kalvin Phillips na Patrick Bamford wapo.

Man-United iko katika orodha ya timu zinazotazamiwa kuwa wawaniaji halisi wa taji la EPL msimu huu.

Walimaliza msimu uliopita wa 2020-21 katika nafasi ya pili, nao wapinzani wao wa leo Leeds waliridhika na nafasi ya tisa.

Mabingwa wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) pamoja na Kombe la Uefa Super Cup, Chelsea, watafukuzia ushindi wao wa nane mfululizo dhidi ya Palace.

Macho yatakuwa kwa straika hodari Romelu Lukaku ambaye amerejea kutoka Inter Milan, na mshambuliaji matata wa Palace, Wilfried Zaha.

Chelsea, almaarufu The Blues, wananolewa na Mjerumani Thomas Tuchel naye Mfaransa Patrick Vieira yuko usukani Palace.

Chelsea walimaliza msimu jana katika nafasi ya nne huku Palace ikilikunja jamvi la EPL ikiwa nambari 14.Liverpool inatarajiwa kumkaribisha kikosini beki matata Virgil van Dijk baada ya kuwa mkekani kwa muda mrefu msimu uliopita.

Reds wa kocha Jurgen Klopp watalenga kudumisha rekodi ya kutoshindwa na Norwich hadi mechi 15.Baadhi ya silaha ambazo Klopp atatumia leo dhidi ya Norwich ni pamoja na Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino.

Kwa upande wa pili Teemu Pukki na Todd Cantwell watakuwa tegemeo kwa wenyeji ugani Carrow Road.

Leo pia itakuwa zamu ya Leicester kufungua msimu itakapopepetana na Wolves, Watford itazipiga dhidi ya Aston Villa nayo Newcastle italimana na West Ham. Everton na Southampton, Burnley dhidi ya Brighton pia ni leo.

You can share this post!

Pigo KCB viongozi Tusker wakifungua mwanya wa alama tatu...

UMBEA: Uvumilivu una kikomo chake, chunga usije ukala...