Vigogo wa kisiasa kutafuta mbinu mpya kusuka miungano bila BBI

Vigogo wa kisiasa kutafuta mbinu mpya kusuka miungano bila BBI

Na CECIL ODONGO

WANASIASA wakuu nchini sasa watalazimika kurejea mezani na kubuni mikakati mipya ya kutwaa urais mwaka ujao baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) jana.

Rais Uhuru Kenyatta, Kinara wa ODM Raila Odinga pamoja na wanasiasa wa muungano wa OKA, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi wamekuwa wakiunga mkono BBI na hata waliivumisha kwenye majukwaa mbalimbali ya kisiasa.

Kwa upande mwingine, Naibu Rais Dkt William Ruto amekuwa mstari wa mbele kupinga BBI, mara nyingi akisema inalenga kubuni vyeo kwa wanasiasa wachache wanaojali maslahi yao ya kibinafsi.

Dkt Ruto na Bw Odinga ambao wanaonekana wapo kifua mbele katika kiny’ang’anyiro cha kuingia ikulu, sasa wana kibarua kigumu cha kuunda miungano mipya kwa kuwa, bila BBI, nyadhifa za maana zilizosalia ni za Urais, Naibu Rais, Maspika wa Seneti na Bunge la Kitaifa na vyeo vya uwaziri.

Mswada wa BBI ulikuwa umependekeza kubuniwa kwa vyeo vya Waziri Mkuu na Manaibu wake wawili. Iwapo BBI ingefaulu mahakamani, nafasi hizo zingetwaliwa na vigogo wa kisiasa nchini kama wangefanikiwa kuunda serikali mwaka ujao.

Kwa sasa, mfumo uliopo wa urais na naibu wake ndio utasalia na wote na inasubiriwa iwapo wanasiasa wakuu wataridhia nafasi zisizo za hadhi ikilinganishwa na zilizopendekezwa katika BBI.

Hata hivvyo, Bw Odinga alionekana kuweka mikakati ya kujivumisha bila BBI alipotangaza kuwa hawatakata rufaa kuhusu uamuzi wa korti katika Mahakama ya Juu.

“Tunataka kumakinikia sana uchaguzi mkuu ujao. Baada ya kushinda kiti cha Urais basi tutarejesha BBI,” akasema Bw Odinga kwenye mahojiano na Redio Namlolwe wiki hii.

Pia, viongozi wa OKA ambao wote wamesisitiza kuwa watakuwa debeni nao wana kazi ngumu kumteua mwaniaji wa Rais na Naibu wake.

You can share this post!

Serikali yapewa siku 7 kuzuia mgomo wa wahadhiri

BBI ilivyotafuna mabilioni ya mlipa ushuru