Vigogo wa KNUT, KUPPET sasa waanza kuhemeshwa

Vigogo wa KNUT, KUPPET sasa waanza kuhemeshwa

Na FAITH NYAMAI

KUNDI la ‘waasi’ limeibuka ndani ya Chama cha Walimu (Knut) na kile cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuoni (Kuppet) ambalo sasa linataka viongozi wa vyama hivyo kujiuzulu.

Kundi hilo linaloongozwa na Bi Martha Omollo, linadai kwamba viongozi wa Kuppet na Knut wameshindwa kutetea masilahi ya walimu.

Walimu hao ‘waasi’ wanasema kwamba Katibu Mkuu wa Knut Collins Oyuu na mwenzake wa Kuppet Akelo Misori wanashirikiana na serikali ‘kunyanyasa’ walimu kwa kuwataka kurejea vyuoni kupata mafunzo ya lazima ambapo watalipa ada ya Sh6,000 kila mwaka.

“Viongozi wa Kuppet ambao wamejitosa kwenye siasa kujihuzuru. Viongozi hao ni Bw Omboko Milemba ambaye sasa ni mbunge wa Emuhaya, Bw Ronald Tonui ambaye ni mbunge wa Bomet ya Kati na na Mwakilishi wa Wanawake wa Bungoma Bi Catherine Wambilyanga,” akasema Bi Omollo.

Kundi hilo pia linataka Bw Misori, mwekahazina wa Kuppet Wicks Mwethi Njenga na naibu katibu mkuu Moses Nthurima kuondoka afisini ‘kwa sababu wamefikisha umri wa kustaafu’.

Bw Misori, hata hivyo, amepuuzilia mbali wito huo huku akisema kuwa ana miaka 58 na hajafikisha umri wa kustaafu.

Kulingana na Bw Misori, katiba ya Kuppet inaruhusu viongozi kuhududimu hadi umri wa miaka 65.

“Katiba ya Kuppet ilifanyiwa mabadiliko mnamo 2017 na sasa inaruhusu viongozi kujihusisha katika siasa,” akasema Bw Misori.

Kundi hilo linadai kuwa Bw Oyuu alikiuka katiba ya Knut hivyo anafaa kujiondoa afisini.

“Sheria ya Knut inasema kuwa chama kinawakilisha masilahi ya walimu wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ufundi. Lakini Bw Oyuu alipoenda kutia saini mkataba na serikali alisema Knut inawakilisha masilahi ya walimu wa shule za msingi pekee,” akasema.

Bi Omollo alikuwa ameandamana na viongozi wa kundi hilo la ‘waasi’ ambao ni Mabw David Mwembei, Timothy Nderitu, Bi Betty Koech na Bi Salvin Munene.

Kundi hilo limetishia kusajili chama pinzani iwapo Bw Misori na Bw Oyuu pamoja na viongozi wenzao watakataa kujiuzulu.

Kundi hilo linasema kuwa walimu hawakushauriwa katika mpango wa kuwataka walimu kujiendeleza kimasomo (TPD).

Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) imewataka kurejea shuleni kusoma kozi sita. Watakuwa wakisoma wakati wa likizo katika baadhi ya vyuo vikuu na kozi moja itachukua kipindi cha miaka mitano na watalipa Sh6,000 kila mwaka.

Kesi ya kupinga mpango huo wa TPD tayari imewasilishwa kortini na Bungeni.

“Walimu wote walioajiriwa na TSC hawatarejea shuleni kwani hatukubaliani na mpango huo wa TPD,” akasema Bi Omollo.

Kundi hilo pia linataka Bunge kupunguza mamlaka ya tume ya TSC ili iondolewe jukumu la kusimamia utendakazi wa walimu.

Kiongozi wa Kundi la Kitaifa la Kusukumiza matakwa ya Walimu, Martha Omollo ahutubia wanahabari kuhusu pingamizi zao dhidi ya mpango wa walimu kujiongeza elimu (TPD), Nairobi, Jumanne. Picha/Hisani

Linasema TSC kwa sasa inatekeleza majukumu mawili; kuajiri walimu na kisha kufuatilia utendakazi wao kwa kuadhibu walimu wanaokiuka maadili.

Walimu hao walidai kuwa TSC imekuwa ikiumiza walimu kwa kutekeleza majukumu hayo mawili.

You can share this post!

Mlipuko wa ugonjwa wa kuhara wazua hofu vijijini Boni

Jamii ya Sengwer yalia viongozi kusahau eneo lao kimaendeleo