Vigogo wapasua kura

Vigogo wapasua kura

Na WAANDISHI WETU

WAGOMBEAJI urais katika uchaguzi ujao huenda wakawa na kibarua kigumu katika ukanda wa Pwani, baada ya mgawanyiko wa viongozi wa kaunti zilizo na idadi kubwa ya kura kufika kileleni.

Juhudi zilizokuwa zikifanywa na viongozi mbalimbali kuwaleta pamoja magavana watatu wenye ushawishi wa kisiasa eneo hilo kabla uchaguzi ujao, zimegonga mwamba.

Hii ni baada ya Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya kutangaza rasmi kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kwa urais.

Bw Mvurya, ambaye baadhi ya viongozi wa Pwani hutaka awe mgombea mwenza wa Dkt Ruto 2022, kwa muda mrefu amekuwa akikwepa suala kuhusu upande atakaoegemea katika uchaguzi wa urais.

Gavana huyo pamoja na mwenzake wa Mombasa, Bw Hassan Joho, na Bw Amason Kingi wa Kilifi, wanaaminika kuwa na ushawishi kwa siasa za Pwani hasa katika kaunti zao.

Bw Joho angali amesimama wima na Bw Odinga, huku Bw Kingi akisubiriwa kuamua kuhusu mgombeaji urais ambaye atamuunga mkono kupitia Chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

Kulingana na takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kaunti hizo tatu zimebeba kura zaidi ya milioni 1.4 kati ya takriban milioni mbili za kaunti zote sita.

Bw Mvurya alitetea uamuzi wake na kusema kuwa, Dkt Ruto anastahili kupewa nafasi kuendeleza mipango ya maendeleo ambayo alikuwa ameanzisha pamoja na Rais Uhuru Kenyatta.

“Wewe (Ruto) ulishiriki katika kuleta maendeleo Kwale kwa hivyo tunasema kazi iendelee,” akasema.

Dalili za gavana huyo kuelekea upande wa Dkt Ruto zilianza kuonekana wakati wa uchaguzi mdogo wa Msambweni mwaka uliopita.

Katika uchaguzi huo, wawili hao waliungana kumpigia debe Bw Feisal Bader, ambaye aliibuka mshindi dhidi ya Bw Omar Boga wa ODM. Bw Boga aliungwa mkono na wanasiasa wa Jubilee wanaoegemea upande wa Rais Kenyatta.

Bw Joho husisitiza kuwa Bw Odinga ndiye anastahili kupewa nafasi ya uongozi, akisema ana uwezo wa kuboresha hali kitaifa kwa manufaa ya wananchi ikilinganishwa na wapinzani wake.

“Wana ajenda gani hawa watu? Sisi ajenda yetu ni kuletea wananchi maendeleo kwa sababu jukumu letu kuu ni kuwakilisha wananchi. Lazima ujihadhari na mtu ambaye anakukumbusha wewe ni maskini. Katika enzi hii 2021 unaniambia suluhu ya matatizo yangu ni wilibaro?” akauliza wikendi, alipokutana na viongozi wa Mombasa.

Alipuuzilia mbali uwezekano wake kuungana na Dkt Ruto baadaye, kufuatia uvumi ulioanza kuenea wakati kakake, Bw Mohamed Amir, alipohamia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) wiki chache zilizopita.

Mapema mwaka huu, magavana hao watatu walikutana na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Mkutano huo wa Machi ulifanyika wakati ambapo mizozano ilizidi kuhusu uundaji wa chama kimoja cha Pwani.

Juhudi hizo zilikuwa zikipingwa na baadhi ya wanasiasa akiwemo Bw Odinga, aliyedai ni hatua itakayoleta vyama vya kikabila.

Bw Kingi ameshikilia msimamo wake kuwa PAA ina nafasi bora kuleta umoja wa kisiasa Pwani, huku akikashifu wanasiasa ubinafsi ndio huwatenganisha kila wakati.

“Kuna mambo mengi ambayo yanakumba watu wetu hapa Pwani ikiwemo suala tata la ardhi. Imekuwa vigumu kutatuliwa kwa sababu ya viongozi kuabiri magari ya watu. Wakati umefika tuwe na gari letu. Hili gari ni chama chetu chenye mizizi yake Pwani,” alisema Bw Kingi wiki iliyopita.

Kufikia sasa, magavana wengine watatu wanaotumikia kipindi cha kwanza cha uongozi wanaegemea upande wa Bw Odinga. Wao ni Gavana wa Taita Taveta, Bw Granton Samboja wa Chama cha Wiper, mwenzake wa Lamu, Bw Fahim Twaha (Jubilee), na Dhadho Godhana wa Tana River ambaye ni mwanachama wa ODM.

Taarifa ya Siago Cece, Valentine Obara na Alex Kalama

  • Tags

You can share this post!

Vyakula vilivyo na madini ya kalsiamu na umuhimu wake...

Tsunami yatikisa ndoa ya OKA

T L