Vigogo wapigania Karua kuunda muungano naye

Na BENSON MATHEKA

MSIMAMO imara wa kisiasa wa kiongozi wa chama cha NARC- Kenya, Martha Karua, umevutia baadhi ya wagombea urais wanaopanga kumrushia chambo wakitaka kumshawishi aungane nao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Tajiriba yake katika siasa na ujasiri wake katika masuala yenye umuhimu wa kitaifa, umefanya jina lake kutajwa na wanamikakati wa wanasiasa wanaopanga miungano ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Ingawa Bi Karua hakujibu tulipotaka kupata kauli yake, wadadisi wanasema kutokana na misimamo yake mikali, wengi wanachukua muda kabla ya kumweleza nia yao na wanatumia kila mbinu kumvutia upande wao.

Wadadisi wanasema kwamba, Bi Karua ndiye anayeweza kuwa mgombea bora mwenza wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Naibu Rais William Ruto amepenya eneo la kati ambapo kampeni yake ya hasla imepata umaarufu mkubwa na baadhi ya duru zinasema kwamba, wanamikakati wake pia wametaja jina la Bi Karua.

Bw Odinga hajatangaza azima ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, lakini kulingana na wandani wake wa karibu, waziri mkuu huyo wa zamani ndiye chaguo la chama cha ODM.

Bi Karua ni mmoja wa wanaopinga Mswada wa Kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), uliosimamishwa na Mahakama Kuu na ambao Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wanaunga.

Inasemekana Bw Odinga anatafuta kiongozi wa kuungana naye kutoka eneo la kati ambapo jina la Bi Karua limetajwa na wanamikakati wake kama njia moja ya kumtaka abadilishe nia ya kuunga mchakato huo.

“Pingamizi kubwa ni msimamo wa Bi Karua kuhusu BBI. Hii imefanya wanamikakati wa Bw Odinga kusita japo wanaamini anaweza kuongeza thamani katika kambi yao ikizingatiwa hana rekodi ya ufisadi,” alisema mbunge mmoja wa ODM aliyeomba tusitaje jina lake asiadhibiwe kwa kufichua mikakati ya chama.

Bi Karua na Bw Odinga wamekuwa wakiunga mirengo tofauti ya kisiasa tangu uchaguzi mkuu wa 2007. Kwenye uchaguzi huo, Bi Karua alikuwa akiunga chama cha Party of National Unity dhidi ya ODM cha Raila Odinga.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bw Mutahi Ngunyi, Bw Odinga akiungana na Bi Karua, watahitaji asilimia 6 pekee ya kura za eneo la Mlima Kenya kushinda urais.

“Kwenye uchaguzi wa 2007, 2013, na 2017, Raila alikuwa na asilimia 44 ya kura. Kwa hivyo, Uhuru akichagua Karua, unafikiri anaweza kukosa kuvutia asilimia 6 ya kura za Mlima Kenya?” ahoji Ngunyi.

Lakini mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo anasema kwamba, japo Bi Karua ni mwanasheria mkakamavu na mwanaharakati mtajika ambaye msimamo wake unavutia wengi, muungano unaoweza kuvutia ni akiwa na Gavana Ann Waiguru na Peter Kenneth upande mmoja.

Anasema sio rahisi kwa Bi Karua kuyumbishwa na mawimbi ya siasa na kubadilisha msimamo wake.

Duru katika chama cha United Democratic Alliance ambacho Dkt Ruto ananuia kutumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, zinasema kwamba, wanamikakati wa naibu rais walianza kumchangamkia Bi Karua kwa kupinga mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI.

“Tatizo limekuwa ni mbinu ya kumshawishi,” alisema afisa huyo na kukata simu.