Vigogo wawania Mlima Kenya kama mpira wa kona

Na NICHOLAS KOMU

KAMPENI za kusaka kura za Mlima Kenya zimechacha, wawaniaji mbalimbali wakitumia mgawanyiko uliopo kujinadi kwa raia, huku ushawishi wa Rais Uhuru Kenyatta ukiendelea kupungua eneo hilo.

Ikiwa inajivunia karibu kura milioni tano, eneo hilo sasa limekuwa kivutio kwa wanasiasa kutoka nje ambao wanalenga kuingia Ikulu mnamo 2022.

Naibu Rais Dkt William Ruto, Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka ni kati ya vigogo ambao wamekuwa wakitua kaunti za mlimani ili kunadi sera zao za kisiasa.

Kutokana na kukimya kwa Rais na kuendelea kwa mpasuko ndani ya Jubilee, Naibu Rais Dkt William Ruto anaonekana amevuna wafuasi wengi huku wabunge wengi wakijiunga na chama chake kipya cha UDA.

Chama hicho kinajivunia umaarufu mkubwa na hata kilishinda katika chaguzi ndogo za Kiambaa wadi za Muguga na Rurii.

Aidha, wabunge wengi wamekuwa wakiendeleza injili ya vuguvugu la Hasla eneo la Kati na kumkashifu Rais kwa kuwarai waunge mkono serikali yake 2013 na 2017 kisha baadaye kutalikiana na Dkt Ruto.

Kwa upande mwingine kumezuka kundi la Kieleweke ambalo limekuwa likiunga mkono ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga kupitia handisheki. Ingawa hivyo, Bw Odinga bado hajaanza ziara za kujitafutia umaarufu eneo hilo ambalo linajumuisha kaunti 14.

Si hayo tu, mgawanyiko zaidi umeibuka baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kutangaza kuwa atakuwa debeni mnamo 2022.

Bw Muturi amepata uungwaji mkono kutoka kwa magavana Kiraitu Murungi (Meru), Martin Wambora (Embu) na Muthomi Njuki wa Tharaka Nithi pamoja na wanasiasa wa Mlima Kenya Mashariki.

Hata hivyo, urais wa Bw Muturi umepingwa vikali na kaunti za Mlima Kenya Magharibi ambazo zina idadi kubwa ya jamii ya Agikuyu.

“Hatuna tatizo la kujiunga na mrengo wowote mradi tu maslahi yetu yamezingatiwa,” akasema Gavana wa Nyeri Mutahi Kagwe wikendi alipokuwa mwenyeji wa Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi.

Katika hafla hiyo, mbunge wa Kieni Kanini Kega naye alishikilia kuwa Rais Kenyatta bado ana ushawishi mkubwa eneo hilo na ndiye atatoa mwelekeo 2022.

“Maamuzi kuhusu 2022 yatafanywa Sagana na ni Rais pekee ambaye atatupa mwelekeo,” akasema Bw Kega ambaye ni jemedari halisi wa mrengo wa ‘Kieleweke’.

Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui naye ametaka mageuzi makubwa yafanywe ndani ya chama cha Jubilee ili kiwe dhabiti kabla ya kura ya mwaka 2022.

“Tukigawanyika basi hiyo itasawiriwa kote nchini. Lazima tuungane na kuhakikisha chama chetu ni dhabiti,” akasema baada ya Kongamano la viongozi wa Mlima Kenya katika Chuo Kikuu cha Methodist wikendi iliyopita.

Bw Moi naye aliwataka wapigakura wa Mlima Kenya wadhihirisha umoja na kuwakagua wawaniaji wote kisha wafanye uamuzi unaofaa wasije wakajuta mnamo 2022.

Kando na hayo, kuna wanasiasa ambao wanamtaka Waziri wa zamani Mwangi Kiunjuri au Bw Muturi, kuwa mgombeaji mwenza wa Dkt Ruto.

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Nasa sinaswi tena