Vihiga Queens kufufua uadui na CBE ya Ethiopia kwenye fainali ya Cecafa kuingia Klabu Bingwa Afrika

Vihiga Queens kufufua uadui na CBE ya Ethiopia kwenye fainali ya Cecafa kuingia Klabu Bingwa Afrika

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Vihiga Queens watamenyana na CBE (Ethiopia) katika fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ya kufuzu kushiriki Klabu Bingwa Afrika jijini Nairobi mnamo Septemba 9.

Vihiga na CBE walitinga fainali baada ya kulima Simba Queens kutoka Tanzania 2-1 na Lady Doves katika nusu-fainali ugani Nyayo hapo Septemba 6.

Maurine Achieng’ na Jentrix Shikangwa walifungia Vihiga mabao yake huku Aisha Mnunka akapachika goli la Simba katika nusu-fainali ya kwanza.

Wachezaji wa Vihiga Queens washerehekea kuingia fainali ya Cecafa. Picha/ Hisani

Katika nusu-fainali ya pili, Loza Geinoire aliweka CBE kifua mbele dakika ya saba kabla ya Fazila Ikwaput kusawazisha dakika ya 61. Hakuna aliyeongeza bao katika muda wa kawaida na kulazimisha dakika 30 za ziada kuchezwa. CBE walijikatia tiketi baada ya kushinda katika upigaji wa penalti 4-3.

Vihiga na CBE walikutana katika mechi za makundi ambapo Waethiopia hao walilemea wenyeji kwa mabao 4-2 mnamo Agosti 29.

Bingwa wa Cecafa atamenyana na wenyeji wa Klabu Bingwa Afrika Wadi Degla SC (Misri) pamoja na AS FAR kutoka Morocco (washindi wa Muungano wa Kaskazini mwa Afrika), AS Mande kutoka Mali (washindi shindano la kwanza la Muungano wa Magharibi mwa Afrika), Hasaacas Ladies kutoka Ghana (washindi shindano la pili la Muungano wa Magharibi mwa Afrika) na Rivers Angels (nambari mbili katika shindano la pili la Muungano wa Magharibi mwa Afrika).

Washindi kutoka Muungano wa Afrika ya Kati kati ya Malabo Kings (Equatorial Guinea) na FCF Amani (DR Congo) pamoja na Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Kusini mwa Afrika (Cosafa) Mamelodi Sundowns Ladies pia wataingia makala hayo ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika ya wanawake yatakayofanyika Novemba na Desemba nchini Misri.

You can share this post!

Waiguru ateuliwa kati ya wanawake 100 bora bara Afrika

CBC yalemea wazazi