Vihiga Queens na Nakuru City Queens wapigana vita vikali KWPL

Vihiga Queens na Nakuru City Queens wapigana vita vikali KWPL

NA AREGE RUTH

VIHIGA Queens waliendelea kusalia kileleni mwa jedwali na alama 16 baada ya raundi ya sita ya mechi za Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL).

Mshambuliaji wa klabu hiyo Janet Moraa Bundi, ambaye alichangia ushindi wa 2-0 dhidi ya Kisumu All Starlets wikendi iliyopita, ni miongoni mwa wafungaji bora kwenye ligi na mabao manne.

Mabingwa hao mara tatu KWPL, hawajapoteza mechi yoyote msimu huu. Wameandikisha ushindi mara tano na kupata sare moja.

Kwa upande wa Kisumu, maji yanaendelea kuzidi unga kwenye timu hiyo. Wameshinda mechi moja na kupoteza nne. Aidha, wameshikilia nafasi ya 10 kwenye jedwali wakiwa na alama tatu.

Vichuna wa Nakuru City Queens ambao wameonyesha ushindani mkali msimu huu, waliwashangaza wengi kwa kuwaadhibu Ulinzi Starlets 3-1 ugani Ulinzi Sports Complex.

Ushindi huo uliwaweka nafasi ya pili kwenye jedwali wakiwa na alama 13. Wamecheza mechi sita wakaandikisha ushindi mara nne, sare moja na kupoteza moja.

Washikadoria nao walishuka hadi nafasi ya nne wakiwa wamezoa alama 10.

Zetech Sparks walivuna ushindi mkubwa wikendi baada ya kuwanyoa Kayole Ladies 5-0 bila maji. Ushindi huo ambao ni wa tatu msimu huu, umewaweka nafasi ya tatu na alama 10. Kayole waliendelea kusalia mkiani bila alama yoyote.

Kwa upande mwingine, Bunyore Starlets pia wameonyesha ushindani mkali msimu huu. Baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Gaspo Women katika uwanja wa Mumboha kaunti ya Vihiga, wameganda kwenye nafasi ya sita wakiwa na alama sita.

Gaspo wana mechi mbili kibindoni na wamesalia katika nafasi ya saba na alama nane.

Msimu huu, Thika Queens wanaendelea kusuasua ligini. Kati ya mechi sita za ligi, wamepoteza mechi tatu na kuandikisha ushindi mara tatu. Walipata ushindi wa 3-0 dhidi ya WADADIA Women siku ya Jumamosi.

Thika na WADADIA wanashikilia nafasi ya tano na nane mtawalia kwenye jedwali.

Magoli 14 pekee yalifungwa wikendi iliyopita. Hii ilikuwa ni idadi ndogo ya mabao ikilinganishwa na michuano ya raundi ya tano ambapo magoli 21 yalifungwa ligini.

  • Tags

You can share this post!

Haaland afunga hat-trick ya nne katika mechi 19 za EPL na...

MUME KIGONGO: Wazee wanywe maji hata wasipohisi kiu –...

T L