Michezo

Vihiga Queens wachupa kileleni Thika Queens wakiwaduwaza Eldoret Falcons

March 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MALKIA wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Kenya (KWPL), Vihiga Queens ilijiongezea pointi tatu na kutua kileleni mwa kipute hicho wakati Thika Queens ikivuna mabao 2-1 dhidi Eldoret Falcons Ugani Eldoret University kutokana na mechi zilizochezwa wikendi.

Nao warembo wa Trans Nzoia Falcons walijikuta njia panda walipochomwa mabao 2-1 na Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) kwenye mechi iliyopigiwa uwanjani Manour Agricutural Centre.

Vihiga Queens ilibebesha Mathare United Women kapu la magoli 8-0 kisha kufunga Nyuki Starlets mabao 2-0. Vipusa hao walinasa ufanisi huo kupitia Terry Engesha na Topistar Situma waliopiga nne safi kila mmoja.

Mwanahalima Adams ambaye pia hupigia timu ya taifa Harambee Starlets na Fauzia Omar kila mmoja alitingia Thika Queens bao moja.

”Nashukuru wachana nyavu wangu kwa kuonyesha ushirikiano mwema dimbani na kubeba alama zote ugenini maana mchezo huo haukuwa mteremko,” bosi wa Thika Queens, Fredrick Chege alisema.

Nayo timu ya GASPO Women iliicharaza Spedag Ladies mabao 3-0 huku Soccer Queens ikipepeta Kayole Starlets magoli 7-1. Leah Cherotich, Winnie Mugechi na Elizabeth Wambui kila mmoja alitikisa nyavu mara moja.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Kisumu Allstars ilikanyanga Vihiga Leeds kwa mabao 6-0, nayo Oserian Ladies ilibamizwa mabao 3-0 na Makolanders huku ikijivunia kushinda mechi mbili wiki iliyopita.

Naye kocha, Rashid Sumba aliongoza Wadadia LG kunasa ushindi wa pili baada ya kuvuna mabao 3-2 mbele ya Mathare United Women.

Kwenye jedwali, Vihiga Queens inaongoza kwa alama 12 baada ya kucheza mechi nne, nayo GASPO Women inafunga mbili bora kwa alama tisa sawa na Thika Queens tofauti ikiwa idadi ya mabao.