Habari Mseto

Vijana 100 walioasi wizi wa mifugo watoa msaada wa mbuzi

February 16th, 2020 1 min read

Na Oscar Kakai

ZAIDI ya vijana 100 walioasi wizi wa mifugo na uvamizi kutoka jamii ya Pokot wanaoishi Kaunti ya Baringo, jana walishangaza wakazi kwa kutoa msaada wa mbuzi kwa waathiriwa maporomoko katika kaunti ya Pokot Magharibi .

Vijana hao ambao walisafiri kutoka eneo la Amaya, eneobunge la Tiaty hadi kijiji cha Chesta, Kaunti ya Pokot Magharibi kupeana kusaidia wenzao walisifiwa na viongozi waliokuwepo.

Maporomoko hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 50 huku wakazi zaidi ya 1,500 wakipoteza makao katika wadi tatu za Batei, Tapach na Weiwei.

Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo ambaye alipokea mbuzi hao alitaja hatua hiyo kama ya kihistoria kwani si rahisi kwa vijana wa jamii ya Pokot kupeana mifugo kwa watu wengine.

Kiongozi huyo alisema kuwa hatua ya vijana hao inaonyesha wamekumbatia mabadiliko, mshikamano na maendeleo baada ya kuasi mila na utamaduni uliopitwa na wakati.

“Vijana hao hawajaenda shule, hawajui Kiingereza wala Kiswahili lakini wana roho ya kusaidia,” alisema Prof Lonyangapuo.

Aliyekuwa mbunge wa Tiaty, Bw Asman Kamama ambaye alikuwa ameandamana nao alisema hatua hiyo itatoa sifa nzuri kwa jamii ya Pokot.