Habari Mseto

Vijana 3,000 washukiwa wa magenge wakamatwa

November 7th, 2019 2 min read

MOHAMED AHMED na FARHIYA HUSSEIN

ZAIDI ya washukiwa 3,000 wanaohusishwa na magenge yanayohangaisha wakazi wa Mombasa wamekamatwa jijini humo huku vita dhidi ya uhalifu vikizidi kupamba moto.

Kamati ya usalama ikiongozwa na Kamishna wa Mombasa, Bw Gilbert Kitiyo ilieleza kuwa vijana hao 3,255 walikamatwa ndani ya muda miezi mitatu.

“Tumekuwa tukiendeleza operesheni za linda salama kwa lengo la kumaliza magenge haramu ya vijana hao majambazi. Tumefanikiwa kuwashika zaidi ya maelfu ya vijana kupitia ushirikiano tuliopata kutoka kwa jamii,” alisema Bw Kitiyo.

Alieleza kuwa wahalifu hao ambao hujihami kwa panga na visu wamekamatwa katika maeneo bunge ya Likoni, Nyali na Kisauni ambapo operesheni hiyo ambayo iliwezesha kupatikana kwa mapanga 255.

Bw Kitiyo alizungumza baada ya polisi mnamo Jumanne kuwakamata vijana 14 kutoka eneo la Bombolulu, Nyali.

Polisi kutoka kituo cha Nyali walikamata washukiwa hao wa genge la Wakali Chee ambalo limekuwa likishirikiana na lile la Wakali Kwanza kuhangaisha wakazi.

Washukiwa hao pamoja na kiongozi wa kundi hilo aliyetambuliwa kwa jina Mwangi walikamatwa na polisi wakiwa katika maficho yao eneo la Vietnam, Bombolulu ambapo pia walipatikana na mapanga 10.

Naibu kamanda wa polisi eneo bunge la Nyali, Bw Simon Thirikwa alisema kuwa washukiwa walipatikana wakiwa wamejificha katika nyumba nne.

“Tulipata fununu usiku wa Jumatatu kuwa kuna vijana ambao wanapanga njama ya ushambulizi asubuhi ya Jumanne. Tulichukulia habari hiyo kwa umuhimu na tukafanikiwa kuwashika vijana hao,” akasema Bw Thirikwa.

Hata hivyo, Bw Thirikwa alisema kuwa washukiwa wengine waliponea na kutoroka mtego huo.

Aliongezea kuwa mapanga yaliyopatikana yalionekana kuwa na damu inayoaminika kuwa ya waathiriwa katika shambulizi iliofanyika wiki mbili iliopita.

“Watu walitoa ripoti kuwa wameshambuliwa na wezi, tutafuatilia uchunguzi na kuangalia sampuli za damu zao kama zitalingana na zile zilizoko kwenye mapanga yaliyopatikana,” akasema Bw Thirikwa.

Magenge yanafahamika sana kwa kuiba na kuchinja watu wa eneo la Kisauni na Nyali.

Aidha, maafisa hao walisema wamejipanga huku msimu wa likizo ukikaribia na watatoa mikakati haswa kuekeza mapolisi eneo la utalii.