Habari Mseto

Vijana 48 nchini huambukizwa ukimwi kila siku – Ripoti

August 27th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

VIJANA 48 wa kati ya miaka 10 na 24 huambukizwa maradhi ya ukimwi kila siku humu nchini huku Wakenya 50, 000 wanaoishi na gonjwa hilo wakifariki kila mwaka.

Hii ni kulingana na utafiti wa Wizara ya Afya wa 2018, ambao umeonyesha kuwa asilimia 15 ya vifo hivyo hutokana na magonjwa yanayovamia mwili kutokana na udhaifu wa kuwa na Virusi Vya Vkimwi (VVU).

Habari hii ilitolewa Jumatatu na mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR) Bi Kagwiria Mbogori, wakati washikadau katika sekta ya afya walipokongamana katika hoteli ya Safari Park Jijini Nairobi kuzindua kongamano la siku tatu kujadili suluhu kwenye matatizo katika sekta hiyo, na namna ya kupunguza maambukizi na madhara ya VVU.

Vikundi kadhaa vikiwakilisha sekta tofauti viliungana kwa nia ya kujadili mageuzi yanayohitajika katika sekta ya afya ili kuinua viwango vya afya nchini na kuwapunguzia wakenya mzigo wa gharama.

“Tunatumai kuwa kongamano hili litaweka wazi jukumu la mashirika ya kutetea haki za binadamu na mabunge katika kutetea haki ya wakenya kupata afya bora, wakiwemo watu wanaougua ukimwi na wengine wenye mahitaji ya muhimu,” akasema Bi Mbogori.

Waziri wa afya Sicily Kariuki alisema mradi wa siku 100 ambao aidha ulianzishwa na wizara yake utasaidia serikali kubaini mapengo zaidi kwenye sekta ya afya, ambayo yamesababisha kuongezeka kwa dawa feki na teknolojia zisizostahili kwenye sekta ya afya.

Alisema uchunguzi wa wizara hiyo pamoja na tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) ulibaini baadhi ya matatizo kwenye sekta hiyo ambayo sasa serikali itakuwa ikijipa jukumu la kuyatatua.

“Tumejua kuwa kuna bidhaa za afya ambazo zinapatikana sokoni ambazo ubora wake ni wa kutiliwa shaka,” akasema waziri huyo.

Alisema serikali inafanya juhudi zote kuhakikisha kuwa gharama ya bidhaa za afya inaenda chini, ili kila mkenya apate haki ya kupokea afya bora kama inavyosema katiba.

“Baada ya kipindi hiki, tunataka wakenya wawe na imani na ubora wa dawa wanazonunua sokoni pamoja na huduma zingine za kiafya,” akasema Bi Kariuki.