Habari Mseto

Vijana eneo la Bangladesh wanufaika na vifaa vya uoshaji magari

July 14th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

VIJANA kutoka eneo la Bangladesh mjini Mombasa wamenufaika na vifaa vya kuendeleza biashara ya kuosha magari.

Vifaa hivyo vilivyofadhiliwa na mwakilishi wadi Bw Renson Thoya, vinapangiwa kuimarisha maisha ya vijana katika mtaa huo wa mabanda.

Siku ya Jumapili vijana hao walipokea mashine ya kuoshea magari, na matangi ya maji ili kuanzisha biashara ya kuosha magari.

Bw Thoya alisema mradi huo utasaidia kupunguza vijana wanaorandaranda katika eneo hilo.

“Kuwapa vijana shughuli kutawasaidia kujiepusha na dawa za kulevya na uhalifu,” akasema.

Alisema kuna haja ya vijana katika mitaa ya mabanda kupewa ujuzi wa biashara ili kujikimu kimaisha.

Aliwaomba vijana kujihusisha na shughuli zitakazowaletea manufaa na kukoma kushiriki uhalifu.

Kiongozi wa vijana hao Bw Amos Ochieng alisema wanahitaji miradi aina hiyo katika mitaa ya mabanda ili kupigana na uchochole.