Habari Mseto

Vijana mashambani wahimizwa watumie fursa na raslimali zilizoko kujiendeleza

November 8th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kubuni ajira zao wenyewe badala ya kutegemea kazi za afisi.

Vijana walioko mashambani wamehimizwa kuanza kilimo bora ili kubadilisha maisha yao.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina alisema dhana potovu ya kufikiri kuwa kazi za afisini ndizo bora inastahili kutolewa akilini mwao na kuzamia katika kilimo kama vile kile cha macadamia na parachichi.

Mkulima wa parachichi eneo la Gatundu Bw Joseph Mwaura aliwashauri vijana wawe mstari wa mbele kuona ya kwamba wanarudi mashambani na kutafuta utajiri kupitia kwa udongo.

“Vijana wengi wametekwa nyara na dhana potovu kuwa wazee ndio wanastahili kuwa mashambani na kuendelea na kilimo huku wao wakiwa mijini wakifanya kazi,” akasema┬áJumamosi akiwa mjini Thika wakati vijana walikuwa wakipewa hamasisho jinsi ya kujiendeleza baada ya kukamilisha masomo katika viwango mbalimbali.

Wakati wa mkutano huo ilielezwa kuwa biashara nyingi za hapa nchini zinaathirika kwa sababu bidhaa nyingi kutoka nchi za nje zinafurika hapa nchini huku zikizuia zile za hapa kukosa soko.

Bw Wainaina ambaye ni mbunge wa Thika, alisema mayai kutoka nchi za nje yamesababisha wafugaji kuku Kenya wasijue ni wapi watapeleka bidhaa hiyo.

“Mwaka 2019 biashara ya maziwa na mayai hapa nchini ilidorora pakubwa huku wafugaji wa ng’ombe na kuku wakiuza bidhaa zao kwa bei ya kutupa,” alisema Wainaina.

Alisema iwapo bidhaa yoyote itaruhusiwa kuingia hapa nchini, itozwe ushuru maradufu ili “kuwapa nafasi hata watu wetu wa hapa nchini nafasi ya kuuza bidhaa zao kwa bei ya kuongeza faida.”

Alisema iwapo vijana watajitolea kuenda mashinani kuendesha kilimo huko bila shaka baada ya miaka mitatu hivi “tunaweza kubuni nafasi za ajira zifikazo milioni moja.”