Habari Mseto

Vijana Samburu wahamasisha jamii kuhusu corona

April 8th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Janga la virusi hatari vya Corona linapoendelea kuzua hofu humu nchini, baadhi ya vijana katika kaunti ya Samburu sasa wamejitwika jukumu la kuhamasisha wakazi wanaoishi mashinani kuhusu njia mwafaka za kujizuia.

Vijana hawa ambao wengi wao ni wa umri wa miaka chini ya 25 wamejitolea kupasha umma habari muhimu na namna ya kujihadhari na virusi hivyo.

Hii ni baada ya Waziri wa afya Mutahi Kagwe kutoa wito kwa vijana kuwa katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya virusi hivyo ambavyo vimewaua watu wapatao sita humu nchini.

Bw Kagwe alisema kuwa ni jukumu la vijana kuweka juhudi na kuzuia maambukizi zaidi humu nchini.

Wakiongozwa na Ann Naishirwa, vijana hawa hutoa huduma za kutafsiri habari muhimu kwa lugha ya kisamburu.

Wengi wa wakazi wa kaunti ya Samburu ambao wanaishi maeneo ya mashinani hukosa huduma muhimu kama vile kupashwa habari.

“Tumeanzisha kampeni ya kutoa hamasa kwa kina baba na mama vijijini na pia kupigana na utoaji habari za kupotosha. Watu wengi hapa hawana ufahamu wa virusi hivi na hiyo no hatari,” alisema Naishirwa.

Naishirwa alisema kuwa wanalenga vijiji ambavyo vimejawa na wazee walio na changamoto za afya kama vile magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu na saratani.

Wiki hii, kundi hili la vijana limejitolea kuelimisha wakazi kuchukua tahadhari zikiwemo kunawa mikono kila wakati, kujitenga wanapohisi dalili za virusi vya Corona na pia kusalia nyumbani.

“Tunaamini kuwa kutoa hamasa kutasaidia kuzuia kuzambaa kwa virusi hivyo mashinani,” aliongeza Naishirwa.

Wiki iliyopita, Waziri Kagwe alionya vijana kuwa wamo katika hatari kupatwa na athari zinazotokana na virusi vya Corona iwapo watashindwa kuchukua majukumu ya kuzuia kuzambaa kwa virusi hivyo.