Habari za Kaunti

Vijana sasa wamulika magavana wakiwataka wawajibike kama wanavyoshinikiza Rais


MAANDAMANO yaliyoshuhudiwa majuzi kote nchini yanayoendeshwa na vijana wa kizazi cha Gen Z yameanza kuzuka mashinani huku baadhi ya vijana wakitaka uongozi bora katika kaunti zao.

Katika Kaunti ya Tana River, vijana sasa wanamtaka Gavana Dhadho Godhana kuwafuta kazi mawaziri wanaoandamwa na kesi za ufisadi na maswali yanayohusu pesa za umma kila mara.

“Kaunti hii imepokea zaidi ya Sh50 bilioni katika muda wa miaka sita iliyopita lakini ukichunguza hakuna chochote kuhusu fedha hizo kando na maafisa wakuu kuendesha magari ya kifahari na mawaziri kujenga majumba ya kifahari,” alidai mmoja wa wasimamizi wa vijana kaunti hiyo,
Hamida Shora.

Waandamanaji hao, walipiga kambi Jumanne na Alhamisi wiki iliyopita na kumkabili Gavana kuhusu mipango ya kuongeza ushuru huku wakazi wakimshinikiza vikali kupitia mitandao ya kijamii.

Katika Kaunti ya Kilifi, Gavana Gideon Mung’aro alilazimika kusitisha kwa muda sheria mpya kuhusu ukusanyaji wa ada katika Daraja la Sabaki kufuatia maandamano.

“Tumejitolea kushiriki mazungumzo yanayoendelea na wadau wote ili kufanikisha utekelezaji na kuhakikisha mazingira bora ya biashara. Tutabuni mikakati ya kupiga jeki ukusanyaji wetu wa mapato ikiwemo kutumia teknolojia na oparesheni usiku na mchana,” alisema Bw Mung’aro baada ya kushinikizwa na umma kwa siku mbili.

Maelfu ya waandamanaji wengi wao Gen Z jana walimkabili Gavana wa Kaunti ya Nandi, Bw Stephen Sang,kuhusu matumizi ya fedha zilizopokewa kutoka Hazina Kuu.

Waandamanaji hao waliobeba mabango walifululiza katika afisi ya Gavana wakiitisha ufafanuzi kuhusu matumizi ya zaidi ya Sh50 bilioni katika hatamu mbili ambapo amekuwa afisini.

“Nimekaguliwa na mamlaka ya kukabiliana na ufisadi, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na ripoti ilionyesha hakuna makosa yoyote na nitahakikisha uwajibikaji na matumizi bora ya fedha za umma,” alisema Gavana Sang.

Baadhi ya kaunti zimesitisha mipango ya kutekeleza Mswada wa Fedha uliopendekezwa ili kuepuka ghadhabu ya waandamanaji wengi wao vijana, kuhusu kutekeleza ada mpya itakayoathiri ukusanyaji wao wa mapato na utoaji huduma.