Michezo

Vijana wa Murunga waanza kwa 'mguu mbaya' London 7s

May 25th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeanza duru ya tisa ya Raga ya Dunia kwa ‘mguu mbaya’ baada ya kuchapwa na Fiji kwa alama 24-17 katika mechi ya kusisimua Jumamosi jijini London, Uingereza.

Vijana wa kocha Paul Murunga walijituma vilivyo katika mchuano huo wao wa ufunguzi wa Kundi B kabla ya kusalimu amri Fiji kupitia mguso wa Paula Dranisinukula dakika ya 13 uliopatikana baada ya Kenya kusalia wachezaji sita wakati Brian Wandera alionyeshwa kadi ya njano.

Fiji, ambayo inashikilia nafasi ya pili kwenye ligi hii ya duru 10, ilitangulia kuona lango kupitia kwa Aminiasi Tuimaba dakika ya kwanza baada ya kuwazidi Wakenya kasi. Livai Ikanikoda aliongeza mkwaju wa mguso huu.

Shujaa, hata hivyo, ilijikakamua na kujibu na mguso bila mkwaju dakika moja baadaye kutoka kwa Bush Mwale, ambaye pia aliwachenga wanavisiwa hawa.

Meli Derenalagi alirejesha Fiji mbele 12-5 alipopachika mguso bila mkwaju sekunde chache baada ya nahodha wa zamani wa Shujaa, Andrew Amonde kunyimwa nafasi ya nzuri sana ya kufunga mguso kutokana na kasi yake ya chini. Hata hivyo, Kenya ilijizatiti na kuhakikisha inaenda mapumzikoni na nafasi nzuri ya kushinda mechi pale Mwale alipopata mguso wake wa pili ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Johnstone Olindi sekunde chache kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika.

Kenya ilijikaza kiume tena na kusawazisha 17-17 kupitia kwa Jeffrey Oluoch baada ya Tuimaba kupata mguso wake wa pili mapema katika kipindi cha pili.

Shujaa ilipata pigo iliposalia watu sita baada ya Wandera kulishwa kadi ya njano na kukaa nje, huku Dranisinukula akifunga mguso wa ushindi.

Ufaransa yanyamazisha Samoa

Katika mechi ya kwanza ya kundi hili, Ufaransa ilinyamazisha Samoa kwa alama 22-14.

Shujaa italimana na Samoa katika mechi yake ya pili hapo saa tisa na dakika 20 kabla ya kukamilisha mechi zake za siku ya kwanza dhidi ya Ufaransa saa kumi na mbili na dakika 26.

Kenya imekuwa ikishiriki ligi hii ya mataifa 15 na timu moja alikwa tangu msimu 2002-2003. Hata hivyo, inakabiliwa na hatari kubwa ya kupoteza nafasi hiyo kwa sababu iko alama nne pekee mbele ya Japan inayoshikilia nafasi ya 15 ambayo mshikilizi wake ataangukiwa na shoka. Vijana wa Murunga wamezoa alama 26 kutoka duru nane za kwanza.

Wanasalia na duru mbili – London (Mei 25-26) na Paris (Juni 1-2) kujiokoa.