Habari MsetoSiasa

Vijana wa NASA wataka Godec aombe radhi kwa 'kumlazimisha' Raila kutambua Uhuru kama Rais

February 15th, 2018 1 min read

Balozi wa Amerika humu nchini Bw Robert Godec. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

VIJANA wa muungano wa NASA wametishia kufanya maandamano ya kushinikiza Balozi wa Amerika humu nchini Robert Godec kumwomba msamaha kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

Vijana hao walimpa Bw Godec makataa ya siku tatu kuuomba msamaha kutokana na kauli iliyotolewa na mabalozi wa mataifa ya Magharibi wakimtaka Bw Odinga kutambua Rais Uhuru Kenyatta kama Rais wa Kenya.

Jumamosi iliyopita, mabalozi 11 wakiongozwa na Bw Godec na  Nic Hailey wa Uingereza walimtaka Bw Odinga kutambua Rais Kenyatta kwani ndiye alichaguliwa kwa mujibu wa katiba.

“Mabalozi wa mataifa ya kigeni haswa Bw Godec wamegeuka kuwa wanasiasa humu nchini. Hatutakubali wageni kuingilia siasa zetu na tumempa siku tatu kuomba msamaha la sivyo tutafanya maandamano katika ubalozi wa Amerika,” akasema David Ochola, kiongozi wa vijana wa NASA.

 

Kutafuta kandarasi

Wakati huo huo, Viongozi wa NASA wakiongozwa na wabunge TJ Kajwang’ (Ruaraka), Simba Arati (Dagoretti Kaskazini), Godfrey Osotsi (Maalumu) na mwanauchumi David Ndii walidai serikali ya Amerika imekuwa ikiunga mkono Rais Uhuru Kenyatta ili kujipatia kandarasi mbalimbali.

“Mwaka jana Balozi Robert Godec alikuwa katika mstari wa mbele katika kushinikiza Amerika kuuzia Kenya ndege za kivita ambazo bei yake iliongezwa maradufu. Kandarasi hiyo imekwama kwa sababu mmoja wa maseneta alisema kuwa kampuni moja kutoka jimbo lake inaweza kuuza ndege hizo kwa nusu ya bei,” akasema Bw Kajwang’.

Wanasiasa hao wa NASA pia walidai kuwa serikali ilitoa kandarasi ya kutengeneza barabara ya kutoka Mombasa hadi Nairobi kwa Amerika siku chache kabla ya uchaguzi wa Agosti 8 kama ‘hongo’ ya kutafuta uungwaji mkono.

“Kampuni moja ya Amerika ilitunukiwa kandarasi ya kukarabati barabara ya Mombasa-Nairobi kinyume cha sheria,” akasema.