Vijana wahimizwa kubuni ajira wenyewe baada ya kupata ujuzi wa kazi

Vijana wahimizwa kubuni ajira wenyewe baada ya kupata ujuzi wa kazi

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA walio na ujuzi wa kozi za kiufundi wamehimizwa kuelewa pia maswala ya biashara na utumizi wa kompyuta.

Pro-Chansela wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) Dkt Vincent Gaitho, alitilia mkazo jambo hilo na kusema kuwa ujuzi wa aina hizo ni muhimu kutokana na ushindani mkali uliopo wa ajira zama za teknolojia.

Aidha, alisema ni vyema kuwa na msimamo kuhusu ujuzi wa elimu ili waliohitimu wawe na nafasi bora ya kupata ajira.

“Serikali na sekta binafsi zinastahili kushirikiana pamoja ili kufanikisha mpango huo,” alifafanua Dkt Gaitho.

Aliyasema hayo kupitia mawasilino ya kimtandao huku akiwarai wazazi kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba wana wao wanapata masomo ya kiufundi na pia ya kibiashara ili kuwa na mafanikio katika ajira.

Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia kwanza biashara za chini kabla ya kufanya zile za juu.

Alitoa wito kwa wanafunzi waliofuzu kuwa na ari ya kujitegemea kwa kubuni ajira wenyewe bila kutegemea sana serikali kuwaajiri.

Alieleza kuwa iwapo kutakuwa na huo mwongozo, bila shaka “tutaonekana kuwa nchi inayoendelea kujitegemea bila kutegemea ujuzi wa kutoka nje.”

Dkt Gaitho aliwataka wazazi wawe mstari wa mbele kuona ya kwamba watoto wao wanafuatilia utaratibu huo kwa makini.

Bw Nick Odhiambo ambaye ni mmojawapo wa wanafunzi waliopata ujuzi wa kozi ya kiufundi, anawahimiza wanafunzi wenzake wafuate mkondo huo ili siku za baadaye wasiwe watu wa kutafuta ajira lakini wajiajiri wenyewe.

“Ujuzi wa pande zote mbili; kuwa na ujuzi wa kibiashara na kuelewa maswala ya kompyuta, ndiyo mwelekeo pekee wa kujiendeleza kimaisha,” alisema Bw Odhiambo.

Mwenyekiti wa Shirika la Sekta Binafsi Nchini – Kenya Private Sector Alliance (KEPSA) – Mhandisi Patrick Obath alisema sekta binafsi pia ina nafasi bora ya kusaidia vijana kuafikia malengo yao ya kupata ajira.

“Iwapo mpango huo utafuatiliwa, bila shaka nchi ya Kenya itatambulika katika kujiendeleza kiviwanda hata ingawa itakuwa ni kwa kiwango cha katikati,” alisema mhandisi Obath.

Alisema cha muhimu ni kwa vijana kujitegemea kwa kubuni kazi wao wenyewe bila kutegemea yeyote.

  • Tags

You can share this post!

Raila abaki jangwani

Magoha azindua mpango wa kutoa msaada wa masomo kwa watoto...