Habari Mseto

Vijana wahimizwa kukuza talanta zao

November 21st, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wanastahili kukuza talanta zao kwa sababu ni tegemeo lao la siku za baadaye maishani.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bi Anne Wanjiku Kibe alisema atahakikisha vijana wenye talanta wanapata nafasi yao inayostahili ili wajiendeleze.

“Tunajaribu kuwaleta vijana pamoja kuona ya kwamba kila mmoja anaonyesha umahiri wake ambao utakuwa kama ngao yao katika maisha. Tuna vijana tofauti kama wanasoka, waigizaji, waimbaji, na hata wasanii na wote hao wana umuhimu wao kimaisha,” alisema Bi Kibe.

Alisema kuna kituo cha kuonyesha talanta kwa vijana katika eneo la Ngorongo,Gatundu Kaskazini, ambacho ni cha kuangazia maswala ya kiteknolojia (ICT), na ni muhimu kwa vijana. Tunataka kuona kila kijana popote pale alipo akionyeshe jambo fulani linaloweza kumsaidia kimaisha,” alisema kiongozi huyo.

Alisema ukumbi huo utakuwa ukitumiwa na vijana ili kuonyesha vipaji vyao huku akitoa mwito kwa kila mmoja kujitokeza bila woga.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jana katika uwanja wa shule ya msingi ya Wandui, Gatundu Kaskazini.

Wakati wa hafla hiyo, mbunge huyo aliwahakikishia vijana kuwa wakati wowote kutoka sasa kampuni ya Avic International inayojenga bwawa la Kariminu itatimiza hakikisho kwamba wataajiri vijana wengi katika mradi huo ili kuwapa nafasi ya kujipatia fedha za kujikimu.

“Kwa muda mrefu vijana wamekuwa wakilalamika ya kwamba hawajapewa kibarua katika mradi huo lakini tayari nimerekebisha mambo na wakati huu vijana kutoka eneo la mashinani wata nufaika na ajira,” alisema Bi Kibe.

Wakati wa hafla hiyo kiongozi huyo aliandamana na Waziri wa Maswala ya Kiteknolojia (ICT), Bw Joe Mucheru na mkurugenzi wa Bodi ya Kudhibiti Filamu Nchini (KFCB) Dkt Ezekiel Mutua ambao walitoa hakikisho kuwa vijana watapewa nafasi kuonyesha talanta zao ili kujiendeleza.

Wakati huo maafisa wa wawili wa michezo Bob Oyugi, na Titus Mulama waliteua wavulana 101 na wasichana 25 ambao watakwenda kufanyiwa majaribio zaidi ya soka ili kugundua talanta zao.

Wanasoka hao walitoka katika timu tofauti kama Mang’u Youth, Nyamathumbi FC, Mwea FC, Igegania FC, Chania North FC, na Chania Raiders FC.

Bw Oyugi ambaye amekuwa katika uwanja wa soka kwa muda mrefu alisema kuna talanta ya kujivunia kutoka kwa vijana hao na kwa hivyo ni vyema kupewa motisha zaidi.

“Mimi na mwenzangu hapa Mulama, tumekuwa tukizuru viwanja tofauti ili kuwasaka vijana wenye vipaji na tayari tumepata kikosi kitakachofanyiwa majaribio zaidi,” alisema Bw Oyugi.