Vijana wakosa nafasi KDF kwa kutumia vyeti feki

Vijana wakosa nafasi KDF kwa kutumia vyeti feki

Na IAN BYRON

MAMIA ya vijana waliojitokeza kusajiliwa katika jeshi la Kenya (KDF) uwanjani Migori, waliamriwa wasishiriki shughuli hiyo baada ya kuwasilisha stakabadhi ghushi.

Shughuli sawa na hiyo ilikuwa imeandaliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Luteni Kanali K M Sayid ambaye alisimamia shughuli hiyo alisema usajili huo ulifanikiwa ila mamia ya vijana waliwasilisha vyeti ghushi wakilenga kujiunga na jeshi kwa njia haramu.

“Shughuli hiyo ilifanikiwa ila tuliwarejesha baadhi ya vijana kwa sababu walikuja na vyeti vilivyoghushiwa,” akasema.

Licha ya kuvumilia kijibaridi kikali na kufika uwanjani humo kwa wakati, vijana wengi walikosa kusajiliwa kutokana na vyeti bandia walivyoviwasilisha. Baadhi yao pia walipatikana na vitambulisho bandia.

Hata hivyo, baadhi ya wenyeji walieleza Taifa Leo kwamba walifungiwa nje ya usajili huo kwa njia zisizoeleweka.

“Licha ya binti yangu kufuzu kutoka Shirika la NYS alikatazwa kujiunga na KDF kwa sababu walisema alama ya vidole haikuwa ikiwiana na kitambulisho chake. Ninashuku hicho kilikuwa kijisababu tu cha kumwondoa,” akasema Bi Jacinter Ouma ambaye aliandamana na mwanawe hadi uwanja huo.

Bw John Ochieng naye alidai mwanawe alifungiwa nje kwa kukosa nakala halisi ya cheti chake cha kidato cha nne. Mwanawe hakuwa amechukua cheti halisi kutoka iliyokuwa shule yake kwa sababu ya kutokamilisha karo. Aliwasilisha cheti cha kumaliza shule pamoja na nakala ya matokeo ya mtihani wake wa KCSE.

Hata hivyo, Kanali Sayid alishikilia kwamba kulikuwa na muda wa kutosha kutimiza mahitaji yote kwa kuwa nafasi za kujiunga na jeshi zilitangazwa mapema mno.

“Aliyefaa kushiriki usajili huu alikuwa akihitajika kuwa na vyeti vyake vya masomo pamoja na stakabadhi nyingine,” akasema.

Matangazo hayo yalitolewa mapema mno na wale ambao hawakuhitimu au kufuzu walikatazwa kujiunga na jeshi,” akaongeza Kanami Sayid.

You can share this post!

Joho apuuza wanaomtaka adandie wilbaro

Mume, 55, achapa mamaye akitaka kujua babaye