Makala

Vijana walioasi Al-Shabaab wasusia mpango wa msamaha wa serikali


IDADI kubwa ya vijana wanaorudi Kenya kutoka Somalia ambako walikuwa wameenda kujiunga na kundi la kigaidi la Al-Shabaab, wamekuwa wakisusia mpango wa msamaha wa serikali.

Imebainika hali hiyo inatokana na kuwa wengi wao hawaamini nia ya serikali.

Mpango huo wa msamaha ulizinduliwa rasmi mwaka wa 2015, ambapo pia ulilenga kuhakikisha kuwa wanaokubali mwito huo na kujitokeza, wanapokezwa mafunzo na ushauri wa kuwafanya kuondoa kabisa itikadi kali akilini mwao, hivyo basi kuishi kama raia wema.

Pia ulinuiwa kuwapokeza ujuzi vijana wahusika na kuwashirikisha kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Naibu Kamishna wa Lamu Mashariki, Bw George Kubai, alikiri kuwa idadi ya wanaokubali mwito huo wa msamaha na kujitokeza bado ni ndogo ilhali mpango huo bado unaendelea.

Aliwasihi vijana ambao walivuka kisiri kurudi Kenya kutoka Somalia na kujificha miongoni mwa jamii kujitokeza wazi kwa hiari na kupokea msamaha wa serikali badala ya kuishi kisiri na kuhatarisha maisha yao.

“Tunawasihi vijana waliovuka Somalia kupokea mafunzo ya itikadi kali na ambao huenda wamebadili nia wakitaka kurudi nchini mwao kuishi maisha ya kizalendo wajitokeze.

“Mlango wa rehema bado haujafungwa. Mwito wa msamaha wa serikali bado upo na ni wa kweli. Wasiogope kujitokeza kwa hiari na tutawasaidia,” akasema Bw Kubai.

Bw Kubai, hata hivyo, alisifu juhudi za serikali katika kupiga vita ugaidi, akieleza kuwa miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa kuimarika kwa hali ya usalama Lamu na nchini kwa jumla.

Aidha, baadhi ya wanaharakati wa kijamii na wakazi waliilaumu serikali kwa kutoendeleza uwazi kuhusiana na mpango huo.

Mkurugenzi wa Shirika la Haki Africa, Bw Hussein Khalid, alisema visa vya mauaji na kutoweka kwa washukiwa wa ugaidi katika miaka iliyopita vilisababisha vijana wengi waliotekwa na itikadi za kigaidi kuhofia kujulikana hata wanapotaka kubadili mienendo yao.

“Kwa maoni yetu, huo mpango wa msamaha wa serikali uliotolewa miaka kadhaa iliyopita umefeli. Haujazaa matunda yoyote na hili linatokana na serikali yenyewe kuvunja mioyo ya wanajamii.

“Kwa sasa jamii haiamini serikali yao. Hawawezi kuwasalimisha vijana wao na kisha wauawe au wapotezwe katika hali isiyoeleweka,” akasema Bw Khalid.

Afisa huyo hata hivyo alipendekeza masuala kadhaa, ikiwemo serikali kuhusisha mashirika ya kijamii, sekta ya dini na ile ya kisiasa katika kuutekeleza mpango huo kwa waliobadili fikra kuhusu itikadi kali na kuwa tayari kubadilika kuwa raia wema.

Bw Ahmed Mzee, ambaye ni mzee wa kijamii Lamu, alisema mpango huo wa msamaha wa serikali utafaulu kutekelezwa endapo utatekelezwa katika njia ya wazi na uwajibikaji.

Anasema kwa sasa ni vigumu vijana kuuamini mpango huo kutokana na kwamba unatekelezwa kwa usiri mwingi.

“Kuna wale waliojisalimisha awali kupokea msamaha wa serikali lakini miaka kadha baadaye, hatujawaona au kusikia kutoka kwao. Serikali nayo iko kimya. Haitaki kuielezea jamii au familia kuhusiana na hatima ya watu wao. Hii ndiyo sababu uoga upo. Vijana hawataki kujisalimisha na kisha kupotezwa au kuuawa katika hali isiyoeleweka,” akasema Bw Mzee.

Kauli yake pia iliungwa mkono na Bi Fatma Yakub, aliyeshikilia haja ya uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza mpango huo wa usalama.