Akili Mali

Vijana waliotaabika bila kazi walivyojijengea viota vya ajira kutoka kwa uyoga

April 17th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

VIJANA waliotaabika bila kazi mjini Bomet wamepata afueni baada ya shamba la utafiti wa mimea kufanywa njia ya kutega uchumi.

Mibey Farm ilianza zaidi ya miaka 10 iliyopita kikiwa kituo cha utafiti wa kuvu kwa kimombo fungi.

Profesa wa Maikolojia, Michael Mibey, baadaye alitoa shamba hilo kwa vijana kulistawisha kiuchumi.

Meneja wa kituo hiki Michael Kipkemoi yuko mstari wa mbele kuhusisha vijana katika uzalishaji wa uyoga.

Kilimo hiki si maarufu sana katika Kaunti ya Bomet lakini umaalumu wake umewachotea pesa wanarika.

“Juhudi za Prof Mibey kufanya utafiti wa makuzi ya uyoga zimesaidia sana kustawisha kilimo na kutoa mafunzo kwa wakulima wapya,” Kipkemoi aliambia Akilimali.

“Tumeandaa mbegu nyingi kwa wakulima nchini ambao wanatafuta miche bora ya kuendeleza zaraa hii,” aliongeza.

Uyoga kukomaa

Kipkemoi anaeleza kuwa ubora wa biashara hii kwamba, mkulima anaweza kuvuna kila siku baada ya uyoga kukomaa.

Mfuko mmoja (kifaa cha kupandiwa) wa uyoga unaweza kutoa mavuno kwa angalau mara saba kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu.

“Wajua uyoga hukua harakaharaka. Leo ukivuna, ukirejea kesho unakuta uyoga umekua tena,” alisema Kipkemoi akitabasamu.

“Kilimo hiki kimefungulia makumi ya vijana nafasi za kazi,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Kipkemoi, kuasisiwa kwa kituo hiki jijini Bomet kumezua haja ya wakazi kutaka kuanza biashara na hata kujumuisha uyoga kuwa chakula nyumbani.

Miongoni mwa shughuli nyingine wanazofanya, ni kuwapandia wakulima wengine uyoga kwenye mashamba yao.

Maandalizi ya shamba

Kazi hii huhusisha kuandaa shamba pamoja na kuhakikisha kuna mazingira mwafaka ya kupanda.

“Soko letu kubwa liko jijini Nairobi katika maduka makubwa licha ya makao yetu kuwa Bomet,” alikiri Kipkemoi.

Uchafu baada ya kumaliza makuzi ya mzunguko mmoja wa uyoga hutumiwa kuwa malighafi ya kuunda karatasi kama vile shashi.

Sasa wako katika mpango wa kutumia taka hizi kuunda bidhaa za karatasi.

Mibey Farm imeibuka kuwa chanzo cha wakulima wengine Bomet kuchangamkia kilimo hiki.

Tangu walipoanza zaidi ya mwongo mmoja uliopita, makumi ya wakulima wamekumbatia zaraa hii ya kipekee.

Ni kilimo kinachohitaji umakinifu wa hali ya juu hasaa kwa kuhakikisha shamba ni safi na hakuna mahudhurio mengi.

Nje ya banda lao kuna dimbwi lenye dawa ambapo wanaoingia shambani hufaa kukanyaga ili kutakatisha miguu.

Harakati hii husaidia kuepuka maradhi yanayoweza kushambulia uyoga.

Vile vile, kabla ya kushughulikia mimea, mkulima anashauriwa kuosha mikono kikamilifu.

Kipkemoi ana matumaini angavu ya kusimamia shamba kubwa la uyoga Kenya mbali na kukuza desturi ya kula na kupanda uyoga.