Habari MsetoSiasa

Vijana wamkemea Rais kuzidi kuwapa wazee kazi

May 22nd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

VIJANA Jumatano walimkemea Msemaji wa Ikulu Kanze Dena kwa kutetea Rais Uhuru Kenyatta kuwa ana mpango mzuri kwa vijana, na kuwa anafanya kila juhudu kutengeneza mazingira na sera nzuri kuwa vijana kunawiri.

Akizungumza kusifu reli ya kisasa (SGR) jinsi imewafaa vijana wengi kwa kuwapa kazi, Bi Dena ambaye aliyekuwa katika kituo cha redio cha humu nchini, alisema vijana wengi wamepata kazi, na kuwa wengi wengine watazidi kupata.

“Rais Kenyatta (pichani) ana mpango mzuri kabisa kwa vijana rohoni. Anafanya bidii kuhakikisha kuwa kuna sera zifaazo na mazingira kwa vijana kukua,” akasema Bi Dena.

Lakini vijana hawakuchukua muda kumkabili, wakishangaa ni kazi gani alizokuwa akizungumzia, wakati Rais akizidi kurejesha wazee wanaostaafu afisini kuwpa kazi za serikali, ilhali anachowapa vijana ni ahadi tu kuwa watajengewa mazingira ya kufanya biashara.

Vijana waliorodhesha wazee kama aliyekuwa makamu wa Rais Moody Awori mwenye umri wa zaidi ya miaka 90 (ambaye Rais alimpa kazi ya kusimamia hazina ya vijana), John Njiraini (ambaye licha ya kukamilisha muhula wa kuhudumu katika mamlaka ya ukusanyaji ushuru KRA bado anaendelea kuhudumu), Francis Muthaura (mwenyekiti wa bodi ya KRA), Joseph Boinnet (aliyekuwa Inspekta Jenerali wa polisi kisha akafanywa waziri msaidizi baada ya kustaafu), miongoni mwa wengine.