Habari Mseto

Vijana wamtaka Sonko awalipe mshahara wa 2018

January 29th, 2019 1 min read

Na SAMMY KIMATU

VIJANA zaidi ya 20 kutoka mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba, South B, Kaunti ya Nairobi wamemtaka gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko kuwalipa malimbikizi ya mshahara wao tangu wafanye kazi kuanzia Agosti 2018.

Vijana hao, wanaojiita Team Abigal kutoka eneo la Kambi Moto walisema waliajiriwa na serikali ya kaunti ya Nairobi katika mradi wa Taka Langu Jukumu Langu.

Fauka ya hayo, walidai wamekuwa wakifanya kazi ya usafi na upanzi wa nyasi katika hospitali ya kujifungulia wamama ya Pumwani na uga wa Nyayo.

Kiongozi wao, Bi Nuria Ali, 32 alisema jana alisema kikundi chake kina wasichana 19 na wavulana sita na licha ya kuchapa kazi ngumu hawajawahi kulipwa hata senti moja.

Kulingana na Bi Nuria, vikundi vili vingine kwenye mradi wa usafi katika serikali hiyo vimekuwa vikipokea mishahara yao bila matatizo.

“Tuna mizozo na wamiliki wa nyumba kwa kukosa kulipa kodi. Huwa wakituona tumevalia sare za kazi tukienda kazini ila hawaelewi ni vipi hatuwezi kulipa kodi. Tunatishwa kufurushwa nje. Wanangu huenda shule wakivalia patipati kwani siwezi kujikimu kuwanunulia viatu,” Bi Nuria akasema.