Habari Mseto

Vijana wanalipa mikopo bila matatizo – Ripoti

June 18th, 2019 1 min read

NA MARY WAMBUI

RIPOTI ya Hazina ya Mikopo ya Vijana (YEF) imeonyesha kwamba idadi ya vijana wanaochukua mikopo hiyo na kuilipa kwa wakati imeongozeka na kuhitimu kiwango cha kuridhisha.

Kulingan na ripoti hiyo, asilimia 88 ya vijana waliochukua mikopo kutoka kwa hazina hiyo wamekuwa wakiilipa bila tatizo lolote.

Kwa muda wa miaka 12 iliyopita, YEF imetoa mikopo ya Sh12.8 bilioni kwa vijana 1,159,393 kutoka maeneo yote nchini.

“Kwa wastani, idadi ya wanaolipa mikopo yao kwa wakati imepanda kutoka asilimia 58 katika mwaka wa kifedha 2015/16 hadi asilimia 88 katika mwaka wa kifedha 2018/19,” ikasema ripoti hiyo.

Katika mwaka huu wa kifedha, Sh549 milioni zilitolewa kwa vijana 109,840 likiwa ongezeko la asilimia 57 ikilinganishwa na fedha zilizotolewa mwaka uliotangulia. Jumla ya Sh518 milioni zilitolewa kama mikopo kwa vijana katika mwaka huu wa kifedha unaokamilika Juni 30.

Bodi hiyo imesifu kuimarika kwa ulipaji mikopo ikisema kutarahisisha kuidhinishwa kwa mikopo mingine kwa vijana wengine, shughuli ambayo ilikuwa ikitatizika awali kutokana na ukosefu wa fedha miaka ya nyuma baada ya vijana wengi kuchelewa kuwasilisha fedha zao.

Mnamo mwaka wa kifedha wa 2016/17, hazina hiyo ilikuwa ikishuhudia idadi ya chini mno ya vijana waliokuwa wakilipa mikopo waliyochukua.

Changamoto

“Hazina imeshughulikia matatizo yaliyokuwa kizingiti kwa utoaji mikopo kwa vijana. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, idadi ya vijana wanaokopa imepanda kwa asilimia 18 huku wanaolipa mikopo kwa wakati pia ikipanda kwa asilimia 30,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa YEF Josiah Moriasi katika ripoti hiyo.

Kwenye bajeti iliyosomwa, Wizara ya Fedha imetengea hazina hiyo Sh335 milioni ambazo zitatolewa kama mikopo kwa vijana kuwasaidia kuwekeza badala ya kutegemea kupata ajira kutoka kwa serikali.

Waziri wa Fedha Henry Rotich pia alisema kwamba hazina ya Uwezo, YEF na Hazina ya Wanawake (WEF) zote zitajumuishwa kuwa hazina moja itayofahamika kama Hazina ya Kibiashara Kenya (BKF).