Habari Mseto

Vijana wanaojihusisha na kamari waitaka serikali isikie kilio chao

July 24th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

MAAJENTI wanaofanya kazi katika kampuni na maduka mbalimbali yanayojihusisha na biashara ya ubashiri na kamari nchini Kenya wameilaumu serikali kwa kutowapa nafasi ya kujieleza kabla ya kuchukua hatua katika sekta hiyo.

Wahudumu hao ambao wengi wao ni vijana walisema hatua ya serikali ya kuzikaba koo baadhi ya kampuni za kamari itakuwa pigo kubwa kwa uchumi.

Hii inajiri siku chache baada ya serikali kuagiza nambari za huduma za malipo – pay bill – na zile za ujumbe mfupi za kampuni hizo zizimwe na kampuni za mawasiliano.

Mamia ya maajenti hao waliozungumza katika eneo la Embakasi walisema kuwa wangetaka kufanya mkutano na Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i ili kuwasilisha malalamishi yao.

“Serikali haijawahusisha washikadau katika sekta hii kabla kuchukua hatua hiyo licha ya kuwa tuko tayari kufanya mazungumzo,” alisema Bw Collins Ochieng.

Waliilaumu serikali kwa kukwaza kile walikiita ni kitega uchumi cha pekee ambacho idadi kubwa ya vijana wasio na ajira ya maana wanategemea.

“Serikali inafaa kujua kwamba idadi ya vijana ambao hawana kazi nchini ni kubwa zaidi ya ile idadi inayokadiriwa na wengi wao kwa sasa wanategemea ubashiri na kamari kujipa kipato,” akasema Bw Mike Baraza anayefanya biashara hiyo katika mtaa wa Embakasi.

Bw Dickson Oktoi ambaye anaendesha biashara hiyo katika eneo la Kitale alisema kuwa kando na wanaobashiri, biashara hiyo imewapa kazi mamia ya vijana.

“Familia za watu wanaofanya kazi katika maduka haya zinawategemea ili kujikimu kimaisha na iwapo watapoteza kazi, litakuwa pigo kubwa,” alisema Bw Oktoi.