Habari Mseto

Vijana wanapeleka hela kwa kamari badala ya kulewa, KBL yalia

April 22nd, 2019 1 min read

Na PATRICK ALUSHULA

KAMPUNI za kutengeneza pombe zimeelezea wasiwasi wazo kuhusu kudorora kwa mauzo kufuatia ongezeko la idadi ya vijana wanaojihusisha na mchezo wa kamari badala ya kujiburudisha na vileo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya mvinyo, Kenya Breweries Limited (KBL) Jane Karuku alisema vijana sasa wanatumia fedha zao katika mchezo wa kutabiri matokeo ya michezo ya soka kwa lengo la kujipatia utajiri wa haraka.

Bi Karuku aliyekuwa akizungumza katika makao makuu ya KBL mtaani Ruaraka, Nairobi, alisema baada ya chakula na kadi za maongezi ya simu, alisema kuwa watengenezaji wa pombe sasa wanakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa michezo ya kamari.

Alisema baada ya chakula na kadi hizo za maongezi katika simu, vijana wa chini ya umri wa miaka 35 wanatumia hela zao za ziada katika kamari badala ya kunywa vileo.

“Siku hizi vibanda ambapo vijana wanakusanyika kucheza kamari ni vingi mno kuliko baa,” akasema Bi Karuku.

“Vijana wengi hupendelea mchezo wa kamari kwani wanaamini hiyo ndiyo njia ya kuwawezesha kujipatia utajiri wa haraka,” akaongezea.

Hivi majuzi, Waziri wa Usalama Fred Matiang’i alisema kuwa zaidi ya vijana 500,000 wameorodheshwa katika taasisi ya kuweka rekodi za watu wanaoshindwa kulipa mikopo (CRB).

Kulingana na Dkt Matiang’i, vijana hao walichukua mikopo na kutumia hela hizo kucheza kamari.

Mnamo 2017, Mamlaka ya Soko la Hisa (CMA) ilisema kuwa michezo ya kamari imewafumba macho vijana na wameshindwa kuwekeza katika soko la hisa.