Makala

Vijana wanavyokwepa kazi za sulubu na kuingilia uuzaji mboga 

Na KALUME KAZUNGU June 25th, 2024 2 min read

WANAUME wengi Lamu, hasa mabarobaro siku za hivi karibuni wameonekana kuchangamkia kazi za kuuza mboga, matunda na bidhaa nyingine kwenye masoko mbalimbali eneo hilo.

Kinyume na dhana ya awali iliyokuwa ikitawala, hasa kwenye mji wa kale wa Lamu kwamba kazi za kuchuuza mboga na matunda ni majukumu ya akina mama, uchunguzi wa Taifa Dijitali umebaini kuwa idadi ya wanaume wanaohudumu kwenye masoko ya Lamu inazidi kuongezeka kila kukicha.

Katika soko la Manispaa ya Mji wa Kale wa Lamu, kwa mdano, idadi ya wanaume ambao wameibukia kazi ya kuuza mboga, matunda na mapochopocho mengine imeongezeka kwa karibu asilimia 50.

Msemaji wa wachuuzi wa soko la manispaa ya Lamu, Abubakar Aboud alisema kati ya wafanyabiashara zaidi ya 300 wa soko hilo, karibu 200 ni wanaume.

Aboud alisema hicho ni kinyume kabisa na miaka ya awali ambapo wanawake sokoni humo walikuwa wengi kushinda wanaume.

Aliweka wazi kuwa vijana wengi, hasa wale ambao awali walikuwa wakitekeleza kazi ngumu, ikiwemo zile za kusukuma mikokoteni, ujenzi na kadhalika miaka ya sasa wamehamia kwenye biashara ya kuchuuza mboga na matunda sokoni.

“Awali, hapa kisiwani hungewapata wanaume wengi wakiendeleza uchuuzi wa bidhaa kwenye soko letu la manispaa. Wanawake ndio walikuwa wengi. Ungepata karibu asilimia 90 ya wachuuzi walikuwa ni wanawake. Miaka ya sasa mabarobaro wamechangamkia kwa wingi biashara ya kuuza mboga sokoni,” akasema Aboud.

Aliongeza, “Kati ya wachuuzi 300 wa hapa sokoni kwetu, utapata wanaume ni karibu 200 idadi iliyosalia ikiwa ni wanawake. Mambo yamebadilika.”

Charles Mwangi, mmoja wa vijana wachuuzi wa mboga na matunda katika soko la manispaa ya Lamu, alisema wanaume wengi wameonelea ni heri kujihusisha na biashara sokoni badala ya kurandaranda bure mitaani bila kazi.

Kulingana na Mwangi, kazi ya kuuza bidhaa, hasa mboga sokoni sio ya kudharauliwa kwani ina pesa.

“Hii kazi yetu ya sokoni ni ya maana. Huwezi kukosa kupata kati ya Sh1,000 na Sh1,500 kwa siku kupitia kuuza mboga, pamoja na viazi, vitunguu na matunda. Ndio sababu vijana wengi wamejiondoa kwenye kazi za sulubu kama vile kusukuma mikokoteni na kujitafutia riziki kupitia uchuuzaji wa bidhaa,” akasema Bw Mwangi.

Katika soko la mji wa Mpeketoni, hali ni ile ile kwani vijana wengi wameibukia uuzaji wa bidhaa sokoni humo.

Soko la mji wa Mpeketoni lina karibu wachuuzi 250, ambapo wengi ni mabarobaro.

Athony Nyagah ambaye awali alihudumu kama bodaboda mjini Mpeketoni, alisema aliafikia kubadili biashara kutoka kwa sekta ya bodaboda hadi uchuuzi wa mboga sokoni.

Anasema siri ya kufaulu, hasa kwenye biashara ya mboga na matunda ni kujihami ni kuwa na vifaa vya kuhifadhi mboga na matunda, kama vile friji, baada ya mchana-kutwa wa kuuza.

“Mimi niliamua kuhama sekta ya bodaboda na kwa sasa nafurahia kuwa mchuuzi sokoni. Nina friji yangu ambayo huitumia kuhifadhi bidhaa zangu, hivyo kuwavutia wateja wanaoona bidhaa zangu zikiwa freshi kila wakati. Uchuuzi wa mboga na matunda una faida si haba,” akasema Nyagah.

Kwa upande wake, Susan Ouma alisifu vijana mabarobaro walioafikia kujiunga nao katika biasharaa ya uchuuzi sokoni akisema walifanya maamuzi mema.

Susan alishauri kuwa nyakati za kubagua kazi kwa misingi ya jinsia, iwe ni ya kike au kiuke zimepita.

Alisema ni kupitia vijana wengi kujitosa kwenye kazi za uchuuzi sokoni ambapo wamesaidika kujiepusha na mihadarati na kushiriki visa vya uhalifu.

“Ukitazama mahali kama kisiwa cha Lamu, idadi kubwa ya vijana wanaotekeleza majukumu ya kuuza mboga sokoni wamefaulu kujinasua kutoka kwa dawa za kulevya. Vijana wasikubali kurandaranda bure mitaani na kuishia kutumia mihadarati. Wajiunge nasi hapa sokoni kama wenzao. Wajue kazi ni kazi,” akasema Susan.