Habari za Kitaifa

Vijana wanne motoni kwa kuigiza wizi wa mkoba na kupakia Tiktok

May 9th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

VIJANA wanne wamekamatwa huku polisi wakimsaka mmoja baada ya washukiwa hao kuigiza wizi wa mkoba wakiwa kwa pikipiki nje ya kituo cha polisi wa utawala (AP) mjini Kilifi mnamo Jumanne jioni.

Miongoni mwa washukiwa hao ni kijana mwenye umri wa miaka 17 na ambaye ni mwendeshaji wa bodaboda.

Polisi pia wanazuilia pikipiki hiyo aina ya Skygo na ambayo ilitumika wakati wa kutengeneza maudhui hayo ya mzaha.

Katika video hiyo, mwanamume anayeigiza kuwa mlevi, anatoka kwenye mkahawa au kantini ya AP na ghafla ananyang’anywa mkoba wake na ‘wezi’ waliokuwa kwenye bodaboda.

Dakika chache baada ya kurekodi video hiyo, washukiwa walisambaza video hiyo kwenye akaunti ya TikTok kwa jiba @shabir-shirazy 003.

Waliipatia video hiyo anwani ya ‘Wezi mbele ya kituo cha polisi’.

Pia iliitwa ‘Mwanaume mwingine aibiwa karibu na kituo cha polisi huko Kilifi’.

Akithibitisha kisa hicho afisini mwake mnamo Jumatano, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini Bw Kenneth Maina alisema polisi waliwakamata wahalifu hao baada ya kuwatambua kupitia kamera ya CCTV katika kantini ya AP Kilifi.

“Video inayoashiria wizi wa wazi tena mchana peupe katika kituo cha AP mjini Kilifi haiakisi ukweli bali ni mzaha ambao vijana walifanya wakitengeneza maudhui kwa akaunti yao ya Tiktok,” akasema Bw Maina.

Aliongeza kwamba vijana hao walikamatwa nyumbani kwao mjini Kilifi, ambapo mshukiwa mkubwa zaidi ni wa umri wa miaka 27.

Kijana mmoja aliigiza kama mwathiriwa wa wizi, mwingine wa umri wa miaka 18 alikuwa akirekodi video hiyo naye mwingine aliigiza kama mwizi. Mwingine wa nne naye alikuwa akiendesha bodaboda.

Bw Maina alisema polisi wanamsaka kijana wa tano.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini Bw Kenneth Maina akihutubia wanahabari mnamo Mei 8, 2024. PICHA | MAUREEN ONGALA

Bw Maina alisema vijana hao walifichua kuwa walitaka kuvutia wafuasi wengi kwa akaunti yao ya TikTok.

“Walikuwa ni vijana watano lakini tumefanikiwa kuwakamata wanne na huyo aliyesalia, tumepata fununu muhimu za kutusaidia kuweza kumkamata,” akafichua.

Kamanda huyo wa Kilifi Kaskazini amehakikishia umma kuwa Kilifi ni pahala salama na haina visa vya uhalifu.

“Tumepata kamera ya CCTV iliyoonyesha jinsi walivyopanga kushuti video hiyo. Umma ufahamu kwamba hakuna utovu wa usalama katika mji wa Kilifi na raia wema wawe huru kufanya shughuli zao za kila siku bila uoga,” akasema.

Aliwataka vijana wa kisasa kuchukua tahadhari na kujiepusha na michezo ya mzaha katika masuala yanayohusu usalama wa raia.

Bw Maina alisema polisi wameanzisha uchunguzi huku akiahidi kuwashtaki washukiwa mara baada ya kukusanya ushahidi tosha.

“Tumeanzisha uchunguzi lakini watashtakiwa kwa makosa tofauti likiwemo la uhalifu wa kimtandao,” akasema.

Kulingana na ripoti ya polisi, Meneja wa Kantini ya AP Kilifi, Bw Roy Otieno, alisema mtu ambaye alikuwa ni mgeni katika mkahawa huo aliomba ruhusa ya kurekodi video eneo hilo lakini akakatazwa.

Licha ya kukanywa, mtu huyo alipuuza na akaanza kurekodi video hiyo ya mzaha na wenzake.