Habari Mseto

Vijana wapanga kuvumisha utamaduni

April 9th, 2018 1 min read

Na KAZUNGU SAMUEL

BARAZA la vijana kuhusu turathi na utamaduni Jumapili lilisema kwamba litaanzisha mikakati kabambe ya kuvumisha utamaduni.

Katibu mkuu wa baraza hilo, Bi Mati Rua, alisema kuwa vijana ndio ambao wanafaa kuchukulia hifadhi ya turathi na tamaduni zao kwa kiwango cha juu kuliko hata mtu mwengine yeyote.

Alikuwa akiongea baada ya kutembelea afisi za Taifa Leo, hapo Jumapili.

“Tunajua kwamba vijana ni wepesi wa kutumia mitandao na teknolojia za kisasa. Na ndio maana katika baraza, tunataka watumie wepesi huo huo kuhakikisha kwamba wanahifadhi tamaduni na maeneo ya turathi,” akasema Bi Mati.

Alisema hivi karibuni, wataanza mikakati ya kukutana na vijana katika kaunti zote 47 ili kuwatumia katika kutoa hamasisho juu ya umuhimu wa hifadhi ya turathi zinazopatikana katika maeneo yao.

“Ukiangalia kwa mfano katika maeneo ya Kaya za Pwani, kumekuwa na visa vya misitu kuharibiwa lakini vijana hawaonekani kujali hilo.

Tunataka sasa kuanza kuwapa elimu ya jinsi gani wanavyoweza kuchukulia kwa umuhimu mkubwa shughuli za kulinda misitu hiyo isiharibiwe.

Vile vile tunataka kuwafunza vijana umuhimu wa wazee katika jamii ili kukabiliana na tatizo la kuuawa kwa wazee na vijana hasa katika maeneo ya Pwani,” akasema.

Baraza hilo lilianzishwa mwezi ulipita katika kongamano la vijana kuhusu turathi na utamaduni ambalo liliandaliwa jijini Nairobi kwa udhamini wa shirika la KNATCOM pamoja na UNESCO.

Mkurugenzi wa utamaduni katika KNATCOM Bw John Omare alisema kuwa mojawapo ya mikakati ambayo inatekelezwa na baraza hilo ni kuwapa fursa vijana kujifahamisha na utamaduni wao.