Makala

Vijana wapiga matari kuamsha Waislamu kuandaa na kula daku

March 29th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAISLAMU kisiwani Lamu wakilala usiku huwa hawana la kuhofia wala kuwatatiza kiakili kuhusu namna ya kuamka kuandaa na kula daku alfajiri.

Hii ni kwa sababu vijana katika kundi mojawapo wamejitolea kuamka asubuhi na mapema kila siku, hasa tangu Ramadhani ianze, ambapo wamekuwa wakizunguka kila mtaa na vitongoji vya mji wa kale wa Lamu wakipiga matari kuamsha waumini wa dini ya Kiislamu kula daku kabla ya saa za mfungo kuanza rasmi.

Daku ni chakula maalumu ambacho huliwa na Waislamu wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Chakula hicho huliwa kabla ya muumini kuanza safari ya saumu mchana mzima kufikia jioni wakati wa kufuturu.

Aidha vijana wa mji wa Kale wa Lamu wamedumisha desturi hiyo ambayo ni ya zamani. Katika miji mingine ya mwambao wa Pwani ya Kenya na maeneo ya bara ambako kuna jamii ya Waislamu, imefifia sana.

Ustadh Mahmoud Abdulkadir Mau alifafanua kuwa wajibu wanaotekeleza vijana hao wa kuamka kati ya saa nane na saa tisa usiku mkuu kuamsha waumini kula daku ni muhimu na unajenga umoja miongoni mwa waja.

“Ni hapa kisiwani Lamu pekee ambapo desturi ya vijana kuzunguka usiku wakipiga vigoma na matari kuamsha Waislamu kula daku imedumishwa. Utawasikia vijana usiku wa manane wakipiga hayo matari wakijua fika kuwa kupitia mpango huo kunao waumini wa dini ya Kiislamu watakaoamka ili kuandaa na kula daku kwa wakati ufaao,” akasema Bw Mau.

Imam Abdulkadir Mau. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alisema mara nyingi vijana wanaotoa huduma hiyo hufanya hivyo kwa kujitolea tu na wala hakuna malipo wanayopewa.

“Pengine muumini aguswe au ajitolee kuwatunuku zawadi au fedha kidogo hao vijana kama shukrani. Ila wanaotekeleza jukumu hilo wenyewe tayari huwa hawatarajii malipo yoyote,” akasema.

Kwa upande wake, Imam Kassim Shee alifafanua kuwa mbali na kuamsha Waislamu kuandaa kula daku, kasida (Qasida) za vijana pia hutuliza mioyo iliyopondeka.

Bw Shee aidha aliwasisitizia wakazi kutoiangalia ‘densi’ ya vijana hao  kama muziki wa kikweli.

“Si muziki vile bali ni kama mashairi au tungo zinazoimbwa kuwaamsha waliolala na pia kuwafanya kutafakari huku wakiamka kula daku. Ni kama kiburudisho au ombi la alfajiri na mapema, hivyo kumweka mja kwenye hali ya kujiandaa mfungo na maombi au swala za siku,” akasema Bw Shee.

Vijana waliozungumza na Taifa Leo walikiri kutekeleza jukumu hilo kwa hiari.

Bw Mohamed Omar, mmoja wa vijana hao, alisema kipendacho moyo ni dawa.

“Katika kukua kwangu, niliwapata wazee wetu wakitekeleza jukumu hili. Nami nikalipenda kwa dhati na ndio sababu hata sasa naendeleza desturi hii muhimu. Ni kama tu tumeirithi hii desturi na tunaifurahia,” akasema Bw Omar.

Kisiwa cha Lamu ni ngome kuu ya dini ya Kiislamu ikilinganishwa na maeneo mengine ya kaunti hiyo.