Habari MsetoSiasa

Vijana washindwa kumzuia Simba Arati kuhutubia

December 17th, 2018 1 min read

Na KNA

KULIZUKA kizaazaa kwenye hafla moja ya mazishi katika Kaunti ya Kisii, baada ya kundi la waombolezaji kujaribu kumzuia mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Bw Simba Arati kufika katika jukwaa.

Bw Arati alizuiwa na kundi la vijana mara tu alipofika katika mazishi ya kakake Mwakilishi wa Kike katika kaunti hiyo, Bi Janet Ong’era katika kijiji cha Igoma, Kaunti Ndogo ya Nyamache.

Vijana hao waliibua kioja baada ya kuzunguka jukwaa ambalo viongozi mbalimbali wa kaunti walikuwa wamekaa.

Hata hivyo, juhudi zao zilizimwa, hivyo kumruhusu mbunge huyo kufika jukwaani.

Bw Arati aliwahakikishia waombolezaji kwamba hakuwa na nia yoyote mbaya, ila alifika kumuaga mwenzake wa ukoo wake.

 

Alirejelea visa vitatu ambapo marehemu alipigwa risasi na kulazwa hospitalini. Aliomba kuhamishwa kwa polisi wanaohudumu katika eneo hilo hadi katika sehemu zingine.

Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni alilalamikia utendakazi wa vifaa vya hospitali vilivyotolewa na serikali ya kitaifa kwa hospitali za kaunti, akisema kuwa vingi havifanyi kazi ifaavyo.

Hata hivyo, alisifia juhudi za Rais Uhuru Kenyatta kukabiliana na ufisadi, akisema kuwa hakuna anayepaswa kusazwa kwenye vita hivyo.