Vijana wazindua kampeni ya kutoa uhamasisho wa uandikishaji kura, Nyanza

Vijana wazindua kampeni ya kutoa uhamasisho wa uandikishaji kura, Nyanza

KENYA NEWS AGENCY na CHARLES WASONGA

KUNDI la vijana wanaompigia upatu kinara wa ODM Bw Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, hapo jana walianzisha kampeni za kuwashawishi watu kujisajili kama wapiga kura.

Kundi hilo kwa jina la Nyanza Youth for Raila (NY4R) lilianza mikakati ya kuwaomba watu wote eneo la Nyanza wajisajili, pindi tu zoezi la usajili awamu ya pili ilipofunguliwa wiki iliyopita.

“ Tulikuwa na hofu kuwa watu wengi wangezubaa na kufungiwa nje ziezi likikamilika tarehe 6 Februari. Kwa hivyo ikatubidi kuwakumbusha ili wengi wajisajili kwa muda unaofaa. Cha kushangaza ni kuwa vijana wengi hawakujisajili katika awamu ya kwanza ya zoezi hili muhimu,” Mwenyekiti wa NY4R, Stanley Lumumba alisema.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ililenga kuwasajili wapiga kura 130,105 katika eneo hilo ila imesajili 5,526 tangu zoezi lilipoanza.

Bw Lumumba alisema kuwa vijana hawajajisajili kwa kutojia ambao unasababishwa na ukosefu wa elimu ya kutosha katika suala la umuhimu wa kupiga kura.

Kampeni hizi za mlango baada ya mwingine unanuia kuwaelimisha wapiga kura kuhusu umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura ili wampigie kura Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha Urais.

“Tunaomba vijana wengi zaidi kwenye maeneo bunge yote ya hapa Nyanza wajisajili kama wapiga kura tunapojitayarisha kwa uchaguzi mkuu ujao. Tutauliza IEBC isambaze vifaa vya usajili katika kila pembe ya eneo hili ili kila kijana apate nafasi ya kujisajili,” alisema.

Wakati huo huo, Jumatatu Bw Odinga alipeleka kampeni zake katika kaunti ya Murang’a ambapo alielezea kuwa ukuruba kati yake na Rais Uhuru Kenyatta utamwezesha uungwaji mkono katika eneo lote la Mlima Kenya.

Bw Odinga pia alitoa wito kwa wawaniaji wa viti mbalimbali kuunga mkono Azimio la Umoja ili wawezesha kushinda viti katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Kutokana na handisheki kati yangu na Uhuru, ninaamini kuwa tutaleta umoja katika taifa letu. Kwa hivyo, nawaomba wale wote wanaogombea viti mbalimbali wajiunge na Azimio ili tuweze kuwa na idadi kubwa ya wajumbe katika mabunge ya kimataifa na mabunge ya kaunti,” akasema.

Kiongozi huyo wa ODM kwa mara nyingine alipuuzilia mbali madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba eneo la Mlima Kenya ni ngome yake akisema sio kweli.

“Watu wa Mlima Kenya sasa wameona mwanga. Wamegundua kuwa yule jamaa ambaye amekuwa akifanya kampeni peke yake kwa miaka minane ni mwongo,” Bw Odinga.

Waziri huyo mkuu wa zamani alisema yeye ndiye anaweza kukamilisha miradi yote ya miundo msingi iliyoanzishwa na rais Kenyatta katika eneo hilo la Mlima Kenya.

“Kwa mfano, nitakamilisha ujenzi wa hii barabara kuu kutoka Kenol kwenda hadi Isiolo hadi kuingia Ethiopia,” akasema.

Bw Odinga alikuwa akihutubu katika eneo bunge la Gatanga ambapo alikutana na wazee wa jamii ya Agikuyu.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Mudavadi ajue Ruto ni sehemu ya serikali...

Matiang’i apuuza kilio cha Naibu Rais

T L