Habari Mseto

Vijana wazua fujo kudai malipo ya Mpango wa Usafi wa mitaa

May 14th, 2020 1 min read

Na SAMMY KIMATU

SHUGHULI katika kituo cha biashara cha South B, eneobunge la Starehe, Nairobi zilikwama kwa muda baada ya vijana kuandamana wakidai malipo baada ya kuhudumu chini ya mpango wa kudumisha usafi mitaani.

Vijana hao zaidi ya 100 waliojawa na hasira walikuwa wakilalama hawajalipwa mishahara yao licha ya wao kufanya kazi kwa wiki moja.

Kulingana na kiongozi wao, Bw Ramon Oduor, waliandamana kufuatia changamoto ya mawasiliano kati yao na maafisa wa utawala eneo hilo.

Mkuu wa tarafa ya eneo hilo, Bw Philiph Mbuvi, alikashifu kitendo hicho akisema baadhi ya wahalifu walitumia maandamano hayo kuwapora wananchi.

Vijana hao walifunga barabara na kuchoma magurudumu, huku kukiwa na mchezo wa paka na panya na polisi.

Naibu kamanda wa polisi eneo la Makadara, Bi Ruth Nyongesa alilazimika kuitisha maafisa zaidi wa kupambana na ghasia na kuagiza vitoza machozi zaidi.