Vijana wengi kuwania 2022 viti vyeo 2022

Vijana wengi kuwania 2022 viti vyeo 2022

Na ALEX NDEGWA

VIJANA WENGI SASA wamejitokeza kuwania viti vya uchaguzi kuelekea kura ya 2022, huku wakiwa na matumaini kwamba wenzao, ambao ndio wengi miongoni mwa wapigakura, watawachagua debeni.

Mnamo 2017, vijana wengi walikuwa wapigakura huku wakijumuisha zaidi ya asilimia 51 – ambayo ni watu milioni 19.6. Idadi yao inatarajiwa kupanda baada ya kukamilika kwa kipindi cha usajili wa wapigakura wapya.

Kati ya watu milioni 1.5 ambao wamesajiliwa kama wapigakura wapya katika zoezi hilo lililotamatika siku chache zilizopita, wengi ni vijana – japo asilimia kubwa walisusia zoezi hilo ikizingatiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ililenga wapigakura wapya milioni sita.

Kutokana kwamba wapigakura wengi ni vijana wa kati ya umri wa miaka 18-35, inamaanishi wakijitokeza kuwania vyeo mbalimbali watachaguliwa kwa misingi ya idadi yao kubwa.Mnamo 2017, vijana 3,428 waliwania vyeo mbalimbali vya uongozi ila asilimia 10 pekee – ambao ni chini ya 314 – ndio walifanikiwa kuchaguliwa.

Gavana wa Nandi Stephen Sang’, maseneta sita, wabunge 20 na madiwani 287 wa mabunge ya kaunti ndio vijana waliochaguliwa.Vilevile idadi ya wawaniaji vijana ambao waligombea viti mbalimbali walikuwa chini ya robo ya wagombeaji wote 14,523 ambao waliwania uchaguzi mnamo Agosti 8, 2017.

Huku uchaguzi mkuu ujao ukikaribia idadi ya vijana ni milioni 14.6 ambayo ni theluthi ya raia wote 47.6 milioni. Watoto ambao wapo chini ya umri wa miaka 18 walikuwa milioni 21.7 mnamo 2019. Pamoja na idadi ya milioni 14.6, inamaanisha kuwa zaidi ya asilimia 76 ya raia wote nchini ni vijana.

Kwenye Bunge la Seneti vijana wametengewa nafasi mbili za uteuzi huku nafasi 12 ambazo ni za Bunge la Kitaifa zikifaa kugawiwa vijana, walemavu na wafanyakazi.Hata hivyo, kizungumkuti ni kuwa vyama vingi vya kisiasa navyo vimekuwa vikiwakazia wawaniaji vijana na kuwapa wakongwe tiketi.

Wanasiasa nao wamekuwa wakiwahadaa vijana kwa kuwapa mapeni machache huku pia wengi wao wakikosa pesa za kufadhili kampeni zao. Kwa mfano mwanasiasa moja ambaye alifanikiwa kuchaguliwa mnamo 2022, alikiri kuwa alitumia jumla ya Sh100 milioni wakati wa kampeni.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa Karuti Kanyinga alieleza Taifa Leo kuwa ni vijana ambao wataamua mwaniaji atakayeshinda kiti cha Urais 2022.

You can share this post!

Lampard ajiondoa kwenye kivumbi cha kuwa kocha mpya wa...

Polisi wapokea mafunzo jinsi ya kukabili ufisadi

T L