Habari Mseto

Vikao vya Seneti kufanyika Kitui wiki ijayo

September 14th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti litaendesha vikao vyake nje ya Nairobi, kwa mara ya pili mwaka huu, katika Kaunti ya Kitui kuanzia Septemba 16 hadi 20.

Kulingana na ilani iliyowekwa kwenye gazeti rasmi la serikali toleo la Septemba 10, na Spika wa bunge hilo, Bw Ken Lusaka, vikao hivyo vitaendeshwa katika majengo ya Bunge la Kaunti ya Kitui.

“Na katika vikao hivyo Seneti itafanya vikao vyake vya kawaida na vya kamati zake kulingana na kalenda yake ya mwaka huu,” akasema Bw Lusaka.

Hoja na miswada kadhaa itajadiliwa katika vikao hivyo kwa siku tano.

Maseneta hao 67 pia watatumia nafasi hiyo kushughulikia masuala yanayowahusu wakazi wa kaunti hiyo ya Kitui inayowakilishwa na Seneta Enock Wambua.

Seneti iliandaa vikao vyake nje ya Nairobi kwa mara ya kwanza katika Kaunti ya Uasin Gishu mnamo Septemba 2018.

Mnamo Alhamisi wiki iliyopita, maseneta walipitisha kwa kauli moja hoja iliyowasilishwa na kiongozi wa wengi, Bw Kipchumba Murkomen, iliyopendekeza vikao hivyo viandaliwe katika Kaunti ya Kitui.