Michezo

Vikosi vitatu vya Stima katika hatari ya kusambaratika licha ya matumaini finyu ya wasimamizi

September 26th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WESTERN Stima, Nairobi Stima na Coast Stima waliopoteza takriban Sh70 milioni mwaka 2020 baada ya kampuni ya umeme ya Kenya Power iliyokuwa ikiwadhamini kusitisha ufadhili, wameapa kusalia ngangari licha ya panda-shuka tele za kifedha.

Wasimamizi wa klabu hizo wamekiri kwamba wanakabiliwa na changamoto za kulipa mishahara ya wachezaji na maafisa wa benchi za kiufundi kwa sasa.

Hata hivyo, wameshikilia kwamba hali itarejea kuwa sawa kambini mwao baada ya wadhamini wapya kupatikana.

“Tumeagana na idadi kubwa ya wanasoka wa haiba kubwa muhula huu. Hata hivyo, hilo halitatutikisa kwa kuwa tunalenga kusajili chipukizi wengi pindi baada ya kupata mfadhili,” akatanguliza mwenyekiti wa Western Stima, Laban Jobita.

“Kikosi kipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na mdhamini mmoja atakayetupa ufadhili wa Sh40 milioni kwa msimu,” akasema kwa kuthibitisha kwamba wameagana rasmi na robo tatu ya wachezaji wao wakiwemo Benson Omalla, Fidel Origa, Maurice Ojwang, Stephen Odhiambo, Kelvin Wesonga, Kennedy Owino, Samuel Njau, Edwin Omondi na Abdallah Wankuru.

Kinara huyo pia amefutilia mbali tetesi kwamba Western Stima, walioambulia nafasi ya saba kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu uliopita, wanalenga kubadilisha jina hadi Keroka Football Club baada ya kupata mdhamini mpya.

Mwenyekiti wa Nairobi Stima, Johnstone Sakwa amesema: “Nashukuru Kenya Power kwa ufadhili wao wa miaka 10. Ingawa tunajitahidi kutafuta mdhamini, hali mbaya ya sasa ya kiuchumi ambayo imechangiwa na janga la corona imefanya baadhi ya mashirika tunayoyafuatilia kusitasita katekeleza maamuzi ya kuwekeza.”

Mwenyekiti wa Coast Stima, David Otieno pia ana matumaini kwamba uchechefu wa fedha unaotishia kuwasambaratisha utawaondokea hivi karibuni na kikosi kusalia thabiti.

Nairobi Stima na Coast Stima waliambulia nafasi za nne na saba mtawalia kwenye Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) msimu uliopita wa 2019-20.

Ushuru FC wanaodhaminiwa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) na Talanta FC inayomilikiwa na Wizara ya Mawasiliano ni miongoni mwa vikosi vingine vinavyofadhiliwa na asasi za kiserikali vilivyopitia hali ngumu ya kifedha.

Huku athari za corona zikizidi kuhisika katika sekta mbalimbali za maendeleo, zipo hofu kwamba baadhi ya vikosi vinavyofadhiliwa na mashirika, asasi na taasisi za kiserikali vitavunjiliwa mbali sawa na hali iliyofanyikia klabu za Pan Paper, Kenya Pipeline, Bata Bullets, Eldoret KCC, Rivatex na Ministry of Works FC.