Michezo

Vikosi vya Chapa Dimba tayari kusafiri Uhispania

May 5th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU za taifa za wavulana na wasichana kwa wasiozidi umri wa miaka 20 ya Chapa Dimba na Safaricom Season Two imezinduliwa tayari kuelekea nchini Uhispania kushiriki mazoezi ya mchezo wa soka.

Vikosi hivyo chini ya kocha, Ted Amumala (Lungari Blue Saints ya Mkoa wa Magharibi) na Paulina Awuor (Acakoro Ladies ya Mkoa wa Nairobi) vitakuwa nchini Uhispania kwa muda wa siku kumi vitakavyoshiriki mazoezi dhidi ya wenzao wa Ligi ya Laliga.

Timu hizo ziliteuliwa kutokana na michuano ambayo imekuwa ikiendelea katika maeneo nane yaliyokuwa mikoa ya taifa hili. Ofisa wa kamati kuu ya Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF), Chris Amimo ameshukuru Safaricom waandalizi wa ngarambe hiyo ambayo ni makala ya pili.

”Bila shaka safaricom inafanya kazi nzuri kutumia mechi hizo kunoa makali ya wachezaji chipukizi mashinani,” alisema na kuwataka wachezaji hao kuwa makini na kujifunza mambo kadhaa kiujuzi kwenye ziara hiyo.

Naye rais wa FKF, Nick Mwendwa alisema ”Kusema kweli migarazano ya msimu huu ilishuhudia ushindani mkali kinyume na ilivyokuwa mwaka uliyopita.”

Kadhalika alisema FKF itazidi kuunga mkono mpango wa Safaricom maana unalenga kupaisha kiwango cha mchezo huo ambao umegeuka kuwa biashara inayosadia wachezaji wengi kote duniani.

Timu ya taifa ya wavulana ya Chapa Dimba na Safaricom Season Two inayotarajiwa kusafiri nchini Uhispania. Picha/ John Kimwere

Timu ya wavulana inajumuisha:John Kato na Saeed Sheikh wote Lungari Saints (Magharibi), Ochieng Owino na Benson Ochieng wa Manyatta United (Nyanza), Ibrahim Abdullah na Abdille Ali wa Isiolo Young Stars (Mashariki), Alex Onchwari wa White Rhino, Abdirahim Mohamed na Marion Idd wa Al Alhy (Rift Valley).

Pia wapo Benson Njenga na Cedric Asmani wa Shimanzi Youth (Mombasa), Mengitsu Lual wa Euronuts na John Mutuma wa Lufa(Mkoa wa kati), Issa Minhaj na Khalid Yusuf wote Berlin FC (Kaskazini Mashariki), Enos Wanyama wa South B United na Lewis Esambo wa Jericho Allstars (Nairobi).

Kikosi cha wanawake: Stella Ahono na Lavenda Murumwa wa Bishop Njenga (Magharibi), Asher Otieno, Carolyne Rufa na Yvonne Ogada wa NCEOD Queens (Nyanza), Nuru Kasiwa na Daisy Chirchir wa St Marys Ndovea (Mashariki), Cynthia Libondo wa Kitale Queens na Claudia Kadenge wa Itigo Girls (Rift Valley), Catherine Aringo na Joy King Lady wote Kwale Starlets (Mombasa), Jane Njeri na Miriam Lutomia wote wa Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati) pia Diana Ambani na Iryne Atieno wote Acakoro Ladies (Nairobi).

Akiongea kwa niaba ya wenzao, Benson Githinji Njenga wa Shimanzi Youth alisema “Katika ziara yetu nalenga kujifunza ujuzi wa kusakata soka ili kuwaonyesha wenzao tukirejea kusudi kuutumia katika fainali za kitaifa.” Fainali za kitaifa zimeratibiwa kuchezwa mwezi Juni mwaka huu uwanjani Kinoru Stadium, Kaunti ya Meru.

Timu zilizofuzu kushiriki fainali ni: Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana (Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens (Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa), wavulana wa Berlin (Kaskazini Mashariki), Barcelona Ladies na Euronuts Boys (Mkoa wa Kati), pia wavulana wa South B United na Acakoro Ladies (Mkoa wa Nairobi).