Vilio Koome aingilie kati kesi za kupinga ufufuzi wa Mumias

Vilio Koome aingilie kati kesi za kupinga ufufuzi wa Mumias

Na SHABAN MAKOKHA

WAKULIMA wa miwa na viongozi katika Kaunti ya Kakamega wamemwomba Jaji Mkuu Martha Koome aingilie kati kesi zinazolenga kuvuruga mpango wa kupokeza mrasimu kampuni ya Sukari ya Mumias.

Kampuni ya Sarrai Group ya Uganda ilishinda kandarasi ya ukodishaji wa kampuni hiyo, kwa miaka 20, lakini hatua hiyo ikapingwa na kampuni ya Tumaz and Tumaz Enterprise Ltd, yake mfanyabiashara Julius Mwale.

Kuna kesi nyingi zilizowasilishwa mahakamani kuzuia ufufuzi wa kampuni ya sukari ya Mumias inayosongwa na changamoto za kifedha.

Bw Mwale alimshtaki meneja mrasimu wa kampuni hiyo Ponangipalli Rao kwa madai ya kutozingatia haki wakati wa kushughulikia zabuni ya kusimamia shughuli za kampuni hiyo.

Kampuni ya Tumaz iliweka zabuni ya Sh27.6 bilioni ili kupewa usimamizi wa mali ya kampuni hiyo huku Sarrai ikitoa Sh11.5 bilioni.

Lakini viongozi kutoka Kaunti ya Kakamega na wakulima wa miwa sasa wanataka kesi hizo zitupiliwe mbali.

Wanadai wale walioelekea kortini wanatetea maslahi yao ya kibinafsi badala ya maslahi ya maelfu ya watu waliotegemea kampuni hiyo kama chanzo cha mapato yao.

Bw Paul Atwa, mkurugenzi wa Pokwise Consultant Group, anasema kuwa maisha yamekuwa magumu katika eneo la Magharibi tangu kampuni ya Mumias ilipositisha shughuli za kutengeza sukari.

Alisema viwango vya umasikini vimepanda katika eneo hilo, kufuatia kusambaratika kwa kampuni.

“Tunashukuru kwa sababu mwekezaji amepatikana kufufua shughuli za Mumias Sugar. Hata hivyo, tunawalaani wale ambao wamekimbia kortini kuzuia shughuli hii kwa sababu kusitishwa kwa shughuli zake kuliathiri watu wengi,” Bw Atwa akasema.

Aliyekuwa waziri wa Michezo, Rashid Echesa aliishauri kampuni ya Sarrai Group kupuunza kesi zilizowasilishwa mahakamani.

“Namtaka mwekezaji huyu mpya kuendelea na shughuli za kufufua kampuni hii ili iweze kuwafaidi wakulima, vijana na wafanyabiashara,” akasema.

“Hata Bw Mwale, ambaye anajenga jiji nyumbani kwao Butere atafaidi pakubwa kampuni hii itakapoanza kutengeza sukari,” akaongeza Bw Echesa.

Mkulima wa miwa, Bw Peter Kalerwa naye alisema kesi zilizowasilishwa kortini zitayumbisha mpango wa ufufuzi wa kampuni hiyo.

You can share this post!

Wafanyikazi wasitisha mgomo Mombasa baada ya kulipwa

Mahakama kuu yazima makadhi

T L