Habari Mseto

Vilio nzige hatari wakiharibu mimea

April 7th, 2020 2 min read

Barnabas Bii na Onyango K’onyango

NZIGE hatari bado wanaendelea kusababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa, huku serikali ikielekeza juhudi zake kwenye viya dhidi ya virusi vya corona.

Tayari, wataalamu wa kilimo wameonya kuhusu hatari ya maeneo hayo kukumbwa na uhaba wa chakula, kwani nzige hao wamesababisha uharibifu wa maelfu ya ekari ya mazao katika zaidi ya kaunti 20.

Serikali imesema kwamba kemikali za kuwakabili zimeisha.

Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wakulima (KFA) Bw Kipkorir Menjo, alisema kuwa kutokana na hilo, nchi inapaswa kujitayarisha kwa uhaba mkubwa wa chakula.

“Wakulima wetu bado hawajapanda mazao yao. Ikiwa nzige watavamia maeneo hayo tena baada ya msimu wa upanzi, basi lazima tujitayarishe kwa uhaba mkubwa wa chakula. Sharti serikali ichukue hatua za haraka kuanzia sasa,” akasema Bw Menjo, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Nzige hao waliripotiwa kuonekana katika maeneo ya Moiben, Sugut, Kabomoi, Chebororwa, Seretyo, Barsombe na Karandili katika Kaunti ya Uasin Gishu. Maeneo hayo huzalisha mahindi na ngano kwa wingi.

Hapo jana, wataalamu walisema kuwa nzige wanahatarisha utoshelevu wa chakula na maisha ya watu katika kaunti zilizoathiriwa, wakitaka hatua za dharura kuchukuliwa kuwazuia kuenea katika kaunti zingine.

“Tumechukua hatua za kutosha kufuatilia mkondo wa nzige hao kwa kuhakikisha kuwa juhudi zinawekwa kuona hawaingii katika maeneo yanayozalisha chakula kwa wingi,” akasema Bw Samuel Yego, ambaye ndiye Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Kulingana na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO), nzige hao wanatarajiwa kutoingia katika kaunti za Uasin Gishu, Trans Nzoia, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi kati ya zingine wakielekea Uganda.

“Tunafuatilia mwelekeo wao na kuchukua hatua zifaazo kudhibiti hali hiyo,” akasema Bi Mary Nzomo, ambaye ndiye Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Kulingana na wataalamu, uvamizi wa nzige hao katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini utaongeza kiwango cha chakula kinachohitajika nchini.

Mashirika Yasiyo ya Serikali (NGOs) ambayo yanashughulikia masuala ya chakula, yanaitaka serikali kuwaeleza wananchi katika maeneo yaliyoathiriwa kuhusu hatua ambazo imechukua kuzuia madhara yanayotokana na kemikali zinazotumiwa kuwakabili.

“Ikizingatiwa kuwa kemikali hizo huenda zikaathiri afya za wale wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa, tunaamini utaratibu unaotumika kuwanyunyizia utaimarishwa ili kutowaathiri wakazi,” yakasema mashirika hayo kwenye taarifa.

Mashirika hayo ni The Route to Food Initiative (RTFI), The Biodiversity and Biosafety Association of Kenya (BIBA-K), Kenya Organic Agriculture Network (KOAN) na Resources Oriented Development Initiatives (RODI Kenya).