Vilio serikali inunue mifugo iliyo hatarini

Vilio serikali inunue mifugo iliyo hatarini

GEOFFREY ONDIEKI na KNA

WAFUGAJI katika maeneo mbalimbali nchini wamelilia serikali kununua mifugo yao ili kuepuka hasara.Katika Kaunti ya Samburu, jamii ya wafugaji imeitaka serikali iharakishe mpango wa kununua mifugo yao ambayo imelemewa na makali ya njaa.

Ng’ombe, ngamia, mbuzi na kondoo katika kaunti hiyo wamedhoofika sana huku wanunuzi wakikosekana nao wale wanaonunuliwa wakiuzwa kwa bei duni.

Jumanne, mamia ya wafugaji ambao walifika katika masoko mbalimbali Samburu kuuza mifugo yao hawakufanikiwa, wakilazimika kuirejesha nyumbani kwa kuwa ilidhoofika sana kiasi cha kutovutia wanunuzi.

Kwa hivyo, wameiomba serikali iharakishe mchakato wa kuwanunua kabla vifo zaidi havijatokea.

“Tunasubiri sana mpango wa kuwanunua mifugo wetu uharakishwe jinsi ambavyo serikali iliahidi. Waharakishe kwa sababu mifugo wetu wanafariki,” akasema Julius Leakono, mfugaji wa ng’ombe.

Wakazi wengi kutoka kaunti kame wamekuwa wakishiriki ufugaji wa kuhamahama na mara nyingi hutegemea mifugo yao kwa mahitaji yao yote ya kimsingi.

Kwa hivyo, vifo vya mifugo hiyo kutokana na makali ya njaa iliyosababishwa na ukame, vimewaathiri mno.

Katika Kaunti ya Samburu, wafugaji wengi wamekuwa wakiwauza wanyama hao ili kuwalipia watoto wao karo ya shule. Hata hivyo, sasa wamepata pigo kubwa kutokana na ukame unaoendelea kushuhudiwa.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (MDMA), bei ya mifugo inaendelea kupungua kwa kasi ya kutisha huku ukosefu wa maji na lishe ukisababisha hali hiyo.

“Mifugo imedhoofika na hali inaendelea kuwa mbaya. Bei ya ng’ombe, ngamia, mbuzi na kondoo nayo imepungua sana na hata wanunuzi wenyewe hawapatikani,” akasema Mshirikishi wa MDMA, Alex Leseketet.

Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Abdul Bahari mnamo Alhamisi wiki jana alisema watasaka soko la mifugo hiyo kutoka Kiwanda cha Nyama (KMC).

Bw Bahari alisema kuwa ununuzi huo utakaoendeshwa na serikali utasaidia kupambana na athari za ukame huo pamoja na uvamizi wa mara kwa mara wa nzige katika maeneo kame.

Huku wakazi wa Samburu wakilia mifugo yao kukosa soko, serikali jana ilianza kuinunua mifugo kutoka wafugaji katika Kaunti ya Kilifi.

Kati ya bajeti ya Sh450 milioni ambayo imetengwa kununua mifugo kutoka kaunti 10 zilizoathirika na ukame huo, Kaunti ya Kilifi imetengewa Sh9 milioni ambazo zimeanza kutumika kununua ng’ombe 450 kupitia KMC.

Ng’ombe 170 na wengine 120 wanatarajiwa kununuliwa katika maneobunge ya Ganze na Kaloleni ambayo yameathirika mno na kiangazi pamoja na ukame.

You can share this post!

TSC yatuza shule, walimu waliofana zaidi masomoni

WASONGA: Vijana wahimizwe kujisajili kwa miradi ya...