Dondoo

Vilio vya demu vyakosa kuzima harusi kanisani

August 21st, 2018 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Kangaita, Kirinyaga

Hafla moja ya harusi kijijini hapa ilisitishwa kwa muda ili kutuliza msichana aliyeangua kilio akilalamika kuwa bibi harusi alikuwa amenyakua mwanamume mpenzi wake.

Mwanadada alidai kwamba jamaa aliyekuwa akifunga pingu za maisha alikuwa mpenzi wake wa miaka mingi, na kwamba alishangaa jinsi mwanadada huyo alivyomnyakua upesi.

Kulingana na mdokezi harusi hiyo iliyoanza kwa utulivu na furaha nusura ivurugike kipusa alipotaka kuelezwa sababu za bibi harusi kumfanyia madharau kiasi hicho ilhali walikuwa marafiki wa dhati.

Inasemekana kidosho alisubiri wakati wawili hao walipokuwa wakivishana pete akazua kioja.

“Huu si utu hata kidogo, huyu ni mchumba wangu ambaye tumekuwa na uhusiano kwa zaidi ya miaka mitatu,” alisema huku akiangua kilio.

Inasemekana kipusa huyo alikuwa akifanya kazi nchi za nje, na kalameni alipomuomba wafanye harusi alidai hakuwa tayari kwa ndoa. Kulingana na mdokezi, demu alitulizwa na baada ya harusi jamaa alieleza sababu za kuoa rafiki yake.

“Nilipokuomba urejee nchini tuoane ulisema haujajitayarisha kwa mambo ya ndoa,” jamaa alimwambia. Hata hivyo, mwanadada alisisitiza bibi harusi alimsaliti.

“Nilisema nitasafiri ili nione huyu msaliti akitiwa pete na mchumba wangu,” aljibu.

Watu walishangazwa na kioja hicho, wengine wakikemea kidosho huyo kwa kukawia kukubali posa ya polo. Hata hivyo, pasta na wazee wa kanisa walituliza mwanadada huyo ambaye aliondoka kwa machungu akiahidi kuhakikisha ndoa hiyo itasambaratika ili mchumba wake amrudie.

“Tutaona kama utaishi na huyu mpenzi wangu,” alionya kipusa. Pasta aliitisha maombi ya kutakasa ndoa ya wawili hao, akikemea matamshi ya msichana huyo.